26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Pogba awaacha njiapanda mashabiki Man United

PogbaMANCHESTER, ENGLAND

KIUNGO ambaye anasubiriwa na mashabiki wa soka wa klabu ya Manchester United, Paul Pogba, amewachanganya mashabiki hao baada ya kudai kwamba anataka kuendelea na klabu yake ya Juventus.

Mchezaji huyo alikuwa jijini New York nchini Marekani kwa ajili ya mapumziko kabla ya kuanza kwa michuano ya Ligi Kuu, lakini alikuwa kwenye rada za klabu mbalimbali ambazo zilikuwa zinamtaka.

Ilidaiwa kwamba, Man United walimalizana na mchezaji huyo kwa hatua za awali ikiwa ni pamoja na kufanyiwa vipimo kwa ajili ya kujiunga na klabu hiyo msimu huu wa usajili.

Juzi mchezaji huyo aliweka picha yake akiwa kwenye ndege anatoka nchini humo na kudai kwamba anaelekea jijini Manchester kwa ajili ya kumaliza suala la uhamisho wake, lakini amewashangaza mashabiki wa United kwa kudai kwamba bado anataka kuendelea na klabu yake ya Juventus katika msimu mpya wa Ligi Kuu.

Pogba akiwa nchini Marekani alipiga picha akiwa na mashabiki wa Juventus ambapo aliweka wazi kuwa ataendelea kuwa na klabu hiyo msimu ujao na kupambana kwa ajili ya kutwaa Klabu Bingwa Ulaya.

Mashabiki hao walimuuliza kama ataendelea kuwa na klabu hiyo msimu ujao, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, alijibu kuwa ndio ataendelea kuwa na klabu hiyo katika msimu mpya wa Ligi Kuu.

Kauli hiyo aliitoa mbele ya mashabiki hao na kupiga picha ya pamoja huku wakionekana wakiwa na furaha kubwa.

Hali hiyo imewafanya mashabiki wa Manchester United ambao wanamsubiri mchezaji huyo wawe na maswali mengi huku wengine wakiamini kuwa atajiunga na timu hiyo muda wowote kuanzia sasa.

Hata hivyo, mtandao wa Sportsmail, unaamini kuwa mchezaji huyo tayari amemalizana na klabu ya Manchester United na kilichobaki ni kumtangaza rasmi.

Mchezaji huyo anataka kuvunja rekodi ya usajili kwa wachezaji wa soka duniani kwa kitita cha pauni milioni 100. Mchezaji ambaye anaongoza kwa kusajiliwa wa fedha nyingi ni mshambuliaji wa Real Madrid, Gareth Bale kwa kitita cha pauni milioni 86 akitokea Tottenham, wakati huo Cristiano Ronaldo akisajiliwa kwa kitita cha pauni milioni 80 akitokea Manchester United na kujiunga na Real Madrid.

Pogba aliwahi kuwa mchezaji wa klabu ya Manchester United kabla ya kuondoka mwaka 2012 na kujiunga na Juventus, lakini kwa sasa anaonekana kuwa lulu katika klabu kubwa za soka duniani, huku akiwindwa na Real Madrid, Barcelona na nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles