WAANDISHI WETU
WAMEREJESHWA. Ndiyo kauli unayoweza kusema baada ya Serikali kuwaruhusu wagombea wote waliochukua fomu na kudhaminiwa na vyama vyao, kushirika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.
Akitangaza uamuzi huo mjini Dodoma jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema wagombea wote waliofanikiwa kuchukua na kurejesha fomu ndani ya muda uliokuwa umepangwa sasa wanapewa sifa ya kupigiwa kura na wananchi wa kijiji,mtaa au kitongoji husika kwa ajili ya uchaguzi huo.
Hatua hiyo, imekuja kutokana na vyama vya upinzani kujitoa kwa madai baadhi ya majina ya wagombea wa vyama vyao mengi yamekatwa.
Jafoo, alisema Serikali imechukua uamuzi huo kwa kuwa imeonekana wazi wananchi kutoka vyama mbalimbali wamekuwa na nia ya kugombea nafasi za uongozi, licha ya vyama vyao kutokuweka umuhimu kuwaelekeza vyema wanachama wao juu ya ujazaji fomu kwa mujibu wa kanuni.
Alisema mamlaka ya uchaguzi imeona ni vyema wananchi wakapewa nafasi ya kushiriki uchaguzi,imejidhihirisha wazi hata baada ya vyama viwili vilivyojitoa bado wanachama wao waliendelea kuwasilisha rufaa zao ili wapewe nafasi ya kushiriki uchaguzi.
“Hakuna kuweka mpira kwapani, mambo yote tarehe 24, kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019, tangazo la Serikali namba 372 la mwaka 2019 kanuni ya 51 ninatoa muongozo wagombwa wote wote ambao waliteuliwa na kudhaminiwa na vyama vyao na kufanikiwa kurejesha fomu za uteuzi kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi.
“Katika kipindi ambacho kimepangwa cha kuchukua na kurejesha wanapewa sifa ya kupigiwa kura na wananchi wa kijiji, mtaa au kitongoji husika kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa,” alisema Jafo.
Alisema majina ya wagombea hayo yatakosa sifa ikiwa siyo raia wa Tanzania, hajajiandikisha kijiji,mtaa au kitongoji husika, amejiandikisha mara mbili, amejidhamini mwenyewe, hajadhaminiwa na chake cha siasa.
Alisema msimamizi wa uchaguzi ameanza kupokea ratiba za kampeni kutoka katika vyama vya siasa kuanzia jana Novemba 10, mwaka huu hadi leo jioni kwa ajili ya kuziunganisha.
“Tarehe na matukio na shughuli zingine zote zinahusu uchaguzi zitaendelea kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa serikali mitaa mwaka 2019,” alisema.
Alisema katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimefanikiwa kupita bila kupingwa maeneo mbalimbali kwa kuwa hapakuwa na mgombea yoyote kutoka chama cha upinzani.
Alisema kwa upande wa wenyeviti wa vijiji, CCM imepita bila kupingwa vijiji 6248 kati ya vijiji 12,319 sawa na asilimia 51.
Alisema upande wa mitaa,CCM imepita bila kupingwa mitaa 1,169 kati ya mitaa 4263 sawa na asilimia 27, huku kwa upande wa vitongoji imepita bila kupingwa katika vitongoji 64,384 sawa na asilimia 58.
“Kwa upande wa wajumbe wa kundi la wanawake,wajumbe 64,085 wamepita bila kupingwa na wajumbe kundi mchanganyiko wajumbe 75,560 wamepita bila kupingwa,”alisema.
Alisema havikatazi vyama kuendelea kujitoa katika zoezi hilo, kwani huu ni uamuzi wao.
NCCR Mageuzi
Akizungumzia kauli ya Jafofo, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema msimamo wao uko palepale mpaka wapate meza ya mazungumzo wala shida yao si madaraka.
“Ndiyo wamesema walionguliwa warejeshwe, je wale waliokosa fomu inakuwaje,”alisema.
Akizungumza mapema mjini Dodoma, Mbatia alitangaza msimamo wa chama cheke kujitoa katika uchaguzi huo kutokana na majina ya wagombea kukatwa.
Alisema majina 35,567 waliyopitishwa na NCCR Mageuzi kugombea nafasi mbalimbali nchini,yaliyorejeshwa ni 149.
Alisema jambo hilo halikubaliki,wameamua kujitoa.
“Baada ya kufanya kikao cha Kamati Kuu, tumeagiza wagombea wetu wajitoe na wadhamini,waliowadhamini ambayo ni matawi, tumegiza waondoe udhamini, au wagombea wajiondoe wenyewe.
” Hatushiriki uchaguzi huu wanatakiwa kufuata kanuni, hatuwezi tukaliacha taifa linapelekwa ovyo, hii ni hatari sana,” alisema.
Alisema kwa mustakabali wa amani ya nchi, vyama vya upinzani vinatakiwa kukaa na Serikali na kujadili sintofahamu ya uchaguzi kwani imekuwa ikiwagawa wengi na inaweza kuleta uvunjivu wa amani.
Alisema ni jambo la kushangaza vurugu kutokea wakati wa kuchukua fomu na hilo linawezekana likawa limetokea Tanzania pekee.
CHADEMA
Alipoulizwa kuhusu kauli ya Waziri Jafo, Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji alisema msimamo wa Serikali umechelewa na kwamba hawabadili msimamo wao.
“Kwa level (uzito wa vikao) uliyotoa umuamuzi na kwa muda uliobaki, si rahisi kubadili haya, tuawatakia kila la heri wafanye uchaguzi mwema,” alisema mashinji.
Muda mfupi kablaya msimamo wa Serikali kulewa, Chadema kilitoa tamko la kumtaka kuacha kutumia nembo na jina la chama hicho kwenye karatasi za uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.
Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika aliwambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alisema anachokifanya ni kinyume na kanuni za uchaguzi ambazo anazisimamia yeye kama waziri wa Tamisemi.
Alisema wanashangazwa kuona Rais Dk. John Magufuli, ameendelea kukaa kimya kutokana na sintofahamu inayoendelea, ikizingatiwa Tamisemi iko chini yake.
“Tunakumbuka rais alijitokeza kwenye uchaguzi huu pale kulipotokea mwitikio mdogo wa uandikishaji akahamasiaha wananchi kujiandikisha, sasa imetokea jambo kubwa zaidi la uchaguzi kuvurugwa ana kuharibiwa yuko kimya, licha ya kelele ambazo ziemendelea kupigwa na viongozi wa dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia.
“Tunamuomba rais ajitokeze azungumze na taifa na akubaliane na rai ambayo imetolewa na Chadema ya uchaguzi kufutwa na rais atangaze kuanza kwa mchakato wa kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi ambayo itapewa mamlaka ya kusimamia chaguzi zote kuanzia ngazi ya kitongoji hadi ya rais,tunamtaka rais ajitokeze yeye na siyo Jafo,” alisema Mnyika.
VIONGOZI WA DINI
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisema mchakato wa uchaguzi huo, usipotendeka kwa haki unaweza kusababisha fujo.
Askofu Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alisema msimamizi mkuu wa uchaguzi huo anayo dhamana ya kuhakikisha uwepo wa ushindani sawa.
“Msimamizi mkuu wa uchaguzi anayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kunakuwa na `fair play’ (usawa) kwa vyama vyote bila upendeleo.
“Zoezi hili lisipofanyika kwa haki linaweza kusababisha fujo na uvunjifu wa amani. Wito wangu kwake na wasimamizi wengine wote wasimamie haki,” alisema Askofu Shoo.
ASKOFU MDEGELA
Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Owdenburg Mdegela alisema ni vizuri wanasiasa kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kupata suluhisho linaloweza kusaidia vyama hivyo kuingia kwenye chaguzi.
“Kwanini wasiahirishe uchaguzi kwanza ili mambo ya siasa yakae sawa?Kujiondoa kwa upinzani mimi nimehuzunika, sikufurahia kabisa kwa sababu tunahitaji upinzani ili mambo yakae sawa.
“Kwa kazi nzuri aliyoifanya Rais Magufuli (John) hili jambo linaweza kuleta doa. Pamoja na ukorofi wa wapinzani bado wanatakiwa kupewa nafasi ya kuingia kwenye uchaguzi,” alisema askofu huyo.
Alionya nchi kwa sasa ikikosa upinzani itasababisha matatizo kidogo na ikiendelea hivi mwakani italeta doa kwenye uchaguzi wa rais na wabunge.
SHEIKH SALUM
Akizungumza na MTANZANIA wakati wa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Mohamad Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alivitaka vya siasa vyama siasa kukaa chini kumaliza tofauti zao ili vishiriki uchaguzi.
Alisema kitendo cha vyama vya siasa kususia uchaguzi ni kuwanyima haki wananchi.
“Hata panapotokea watu kutoelewana katika uchaguzi ni vyema pande zote kukaa chini kumaliza tofauti zao, kitendo cha vyama kutoshiriki uchaguzi ni kuwanyima wananchi haki yao ya kuchagua mtu wanayemtaka,” alisema Sheikh Mussa.
Aliwatakwa wananchi kujitokeza kushiriki uchaguzi huo na kutambua Serikali imara huanzia chini kwa kuchagua viongozi wazalendo, wanaojituma na watakaokuwa tayari kulinda rasilimali za nchi.
Alisema kila Mtanzania anapaswa kuona anao wajibu wa kushiriki uchaguzi na kutambua kuchagua viongozi ni ibada.
”Lazima tushiriki kuchagua viongozi wetu, tuchague viongozi wenye sifa na katika hili tuhakikisha tunachagua salama na amani na kwa kuangalia taratibu za nchi tulizojiwekea.
“Kutoshiriki uchaguzi ni kutoa nafasi kwa mtu mwingine kukuchagulia mtu usiyemtaka,nawaomba wananchi kuona sababu ya kushiriki uchaguzi huo,” alisema Sheikh Mussa.
Kauli ya Jafo
Katika kauli yake juzi jijini Dodoma, Jafo alisema kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa hata kama chama husika kimegoma kushiriki uchaguzi, lazima jina la mgombea lililoteuliwa kushiriki litabandikwa kwenye karatasi ya uchaguzi.
“Chaguzi utaendelea kama kawaida na kile chama kinachotafsiri demokrasia kinachoitaka, huwezi kulazimisha chama kufanya demokrasia ile unayoitaka wewe. Kwa vyama vilivyojitoa ni uhuru wao kidemokrasia, nivishukuru vyama 11 vilivyosema vitashiriki kwasababu ni muda wao wa kujimwambafai.
“Kwa mujibu wa kanuni, mtu akishateuliwa jina linabaki kwenye karatasi ya uchaguzi hata kama kajiengua mwenyewa,” alisema Jafo na kuongeza zaidi ya rufaa 13,500, zimewasilishwa na vyama vya siasa kwenye Kamati za Rufaa za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
ACT WAZELENDO
Taarifa kutoka mkoani Kigoma,zinasema Chama cha ACT Wazalendo kimetoa agizo kwa wagombea wa nafasi za uenyekiti na ujumbe wa Serikali za Mitaa kuandika barua za kujitoa.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Mkoa Kigoma, Ibrahim Sendwe alitoa agizo hilo, wakati wa mkutano wa wagombea wote wa Jimbo la Kigoma Mjini uliofanyika Ujiji.
Alisema chama kimefuta udhamini wake kwa wagombea,hawana haki ya kushiriki uchaguzi huo.
Alisema ili kutimiza matakwa ya kidemokrasia wagombea wote wanapaswa waandike barua za kutoshiriki uchaguzi huo ili majina yao yasiorodheshwe kwenye fomu za wagombea wakati uchaguzi utakapokuwa unafanyika.
Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo, ni mwenyekiti wa kitongoji katika mamlaka za miji midogo, mwenyekiti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa,(kundi mchanganyiko la wanawake na wanaume) na wajumbe wa kamati ya mtaa (kundi la wanawake) katika mamlaka za miji.
Nafasi zingine, ni mwenyekiti wa kijiji,wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji,(kundi mchanganyiko wanaume na wanawake),wajumbe wa halmashauri kuu ya kijiji (kundi la wanawake), wenyeviti wa vitongoji katika mamlaka za wilaya.
Imeandikwa na Ramadhan Hassan (Dodoma), Leonard Mang’oa na Faraja Masinde (Dar) na Editha Karlo (Kigoma).