CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
IMEKUWA ni kawaida kwa madereva na makondakta kuruhusu wapiga debe kuwahi siti kisha kuuza kwa abiria. Jambo hili linataka kujenga mazoea ili lionekane kama ni la lazima.
Mtindo huo mchafu umeenea na kuota mizizi zaidi katika kituo cha daladala cha Mnazi Mmoja.
Wapiga debe hao mara ifikapo jioni lazima utawakuta wamejaa katika stendi hiyo na baada ya mabasi kufika wao ndio huwa wa kwanza kuingia ndani ya magari, kisha kudai Sh 500 kwa kila wanaemwachia siti.
Hii imekuwa ni neema kwa abiria ambao wana fedha lakini wanashindwa kugombania magari, wanapofanikiwa kupanda daladala husika huzinunua siti hizo kwa gharama ya Sh 500 na kuendelea na safari, lakini jambo hili limekuwa kama unyanyasaji kwa wasio na kipato. Maana wanagombania daladala lakini wanakosa sehemu za kukaa na wanashindwa kununua zile zilizowahiwa na wapigadebe.
Ifike wakati kila mwananchi akatambua haki zake za msingi na kuona hana sababu ya kumlipa mpiga debe.
Kumlipa mpigadebe ni sawa na kuwanyima wengina haki zao za msingi hali inayochangia pia kuendelea kuchochea ongezeko la wapiga debe vituoni.
Hakuna asiyefahamu kero kubwa wanayoipata abiria katika vituo vya daladala.
Ni wakati sasa kwa halmashauri na viongozi wa vituo vya daladala kuona umuhimu wa kuwaondoa wapiga debe hao ili kuleta usawa na amani vituoni.
Oparesheni ya kuwaondoa wapiga debe hao imekuwa ikifanyika mara kwa mara lakini baada ya muda mfupi hurejea na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Zipo biashara nyingi katika vituo hivyo, ambavyo wakiamua nao wanaweza kufanya ili kuepuka kazi wanayoifanya sasa. Sasa basi, ni muhimu kundi hili likapewa hata elimu ya ujasiriamali ili waondokane na kazi hiyo.
Hakuna asiyefahamu kila mtu anatafuta riziki, kulingana na eneo lake husika, lakini utafutaji wa wapiga debe umekuwa ni maumivu kwa wengine.