BEIJING, CHINA
SERIKALI ya China imesema bado inapanga kutuma ujumbe wake Marekani kufanya mazungumzo ya biashara licha ya tishio la Rais wa taifa hilo, Donald Trump.
Trump aliapa kuongeza kodi za bidhaa kutoka China baadaye wiki hii, kitisho ambacho kimeathiri masoko ya hisa.
Trump alitoa kitisho hicho wakati wajumbe wa pande zote mbili wakijiandaa kukutana Washington kesho kwa kile kinachoonekana kuwa duru la mwisho la mazungumzo ya kufikia muafaka ama afufue upya vita ya biashara.
Trump amesema kodi ya bidhaa za China za thamani ya dola bilioni 200 zitapandishwa kutoka asilimia 10 hadi 25 Ijumaa wiki hii.
Licha ya hayo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Geng Shuang amesema timu yao kwa sasa inajiandaa kwenda Marekani kushiriki mazungumzo lakini hajaeleza kama mjumbe mkuu wa timu hiyo Liu He atauongoza ujumbe huo au la.
Geng amesema hatua nzuri imepigwa katika duru 10 za mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika na kuwa dunia nzima unafuatilia.