Na MALIMA LUBASHA-SERENGETI
SERIKALI imesema inatambua na kuzifanyia kazi changamoto za wanyama mbalimbali wakiwamo Tembo kutoka Hifadhi ya Serengeti kuvamia makazi ya watu na kufanya uharibifu au kujeruhi na hata kusababisha vifo.
Pia imesema migogoro ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na tozo za kuingia ndani za hifadhi hizo zinashughulikiwa kwa haraka ili kupata mwafaka.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani,wakati akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Serengeti katika ziara yake ya kikazi ya siku moja wilayani humo.
Makani alikiri Serikali kuwa na taarifa ya changamoto hizo kuhusu malalamiko ya wananchi ya tembo kuvamia makazi yao na kula mazao na kusababisha mauaji ya watu na mifugo hivyo inafanya kila linalowezekana kutoa kifuta machozi.
“ Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, imeahidi kutekeleza ahadi zote zinazowakabili wananchi na inapenda wanaoishi jirani na hifadhi kuishi kwa usalama na amani na kunufaika na hifadhi hiyo kwani wao ndio walinzi wa kwanza wa rasilimali zilizomo,”alisema.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Serengeti, Vicent Nyamasagi, alisema changamoto nyingine iliyopo ni tozo wanazotozwa watalii wanaoingia ikiwa ni pamoja wananchi kwamba imezorotesha utalii.
Nyamasagi aliomba Serikali kuingilia kati mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na wananchi ambapo Tanapa imeamua kuchukua maeneo ya wananchi bila kuwashirikisha jambo ambalo limeleta migongano.