Na ROSE CHAPEWA, MBEYA
WANAUME 111 mkoani Mbeya wameripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili, huku wengine 14 wakidaiwa kufanyiwa ukatili wa kingono na wenza wao.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Yahya Msuya alisema hayo wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Alisema katika matukio 2,890 waliyopokea katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya , kwa kipindi cha mwaka mmoja, hali ilikuwa tofauti na ilivyozoeleka.
Alisema, hivi sasa wanaume wamekuwa na mwamko wa kutoa taarifa za kufanyiwa ukatili wa kimwili na kingono na wanawake, lakini ukatili wa kipigo unachukua nafasi kubwa.
“Watu wengi wamezoea kuwa wanaofanyiwa ukatili ni wanawake tu, sasa hivi hali imekuwa tofauti kati ya matukio 451 ambayo tumeyapokea katika hospitali yetu, matukio 111 ni ya wanaume kufanyiwa ukatili wa kimwili.
“Hivyo utaona kuwa sasa hivi elimu tunayoitoa watu wameanza kuelewa na aibu imeanza kutoweka ,sasa wanaume wanaleta taarifa,” alisema Dk. Msuya.
Alisema kutoka na matukio hayo, matukio 1491yalikuwa ni ukatili kwa watoto na kwamba wote waliofanyiwa ukatili wa kijinsia, baada ya kuwafanyia uchukunguzi wa kidaktari baadhi walibainika kuwa na maambukizi ya VVU.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alisema katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2015 walipokea matukio ya unyanyasi wa kijinsia wa kingono 1281na kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu walipokea matukio ya aina hiyo 661.
“ Katika haya matukio ambayo yameripotiwa hapa kwetu , matukio ya ukatili wa kingono yameonekana kuchukua nafasi kubwa sana, lakini tunashukuru yanazidi kuripotiwa , inaonesha kuwa sasa hivi jamii imekuwa na mwamko mkubwa sana wa kutoa taarifa, na kufahamu yale wanayofanyiwa” Alisema Kidavashari.
Aliwaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na taarifa za siri pale wanapoona wanafanyiwa vitendo vya kikatili ili kusaidi wahusika kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Naye Afisa wa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya Haika Temu alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita wa 2015/16 ,ofisi yake ilipokea matukio 400, ambayo yalihusiana na masuala ya utelekezwaji wa familia.
Alisema akina mama wengi walikuwa wakilalamikia wenza wao kuwaachia watoto bila msaada wowote wa matunzo na wengine kutelekezwa bila kujua wenza wao walipo.