Na Clara Matimo, Mtanzania Digital
JITIHADA za kuwawezesha kiuchumi wanawake na vijana nchini zinazidi kupiga hatua ambapo jumla ya wanawake na vijana 3,227 katika vikundi 300 kutoka mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro na Njombe wamewezeshwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Makundi hayo yamewezeshwa kupitia mradi wa Mwanamke Imara wenye lengo la kutokomeza aina zote za ukatili wa kijinsia unaotekelezwa kwenye mikoa hiyo na mashirika manne ambayo ni Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania(TAWLA), WILDAF, KWIECO na TANLAP Kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Afisa Mradi huo kutoka Shirika la Kwieco, Peter Mashingia wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani Kilimanjaro waliokuwa kwenye ziara ya kuona changamoto na mafanikio ya mradi huo.
Mashingia alisema wanufaika hao wamepewa mafunzo ya usimamizi wa shughuli za ujasiriamali, ujuzi kwenye mipango na uendelevu wa biashara, utunzaji fedha, uanzishaji biashara, namna ya kuimarisha ujuzi katika masuala ya kuongeza thamani kwenye bidhaa za kilimo, ufugaji wenye tija na masuala yote ambayo yanaweza yakatafsiri ustawi wa mwanamke na kijana kwenye kufanya shughuli za ujasiriamali zenye tija.
“Tumejifunzakwamba asilimia kubwa sana ya wanawake na vijana walioimarisha vipato vyao wana nafasi kubwa ya kupunguza utegemezi na utegemezi ukipungua miongoni mwao kwa asilimia kubwa sana hatari za ukatili wa kiuchumi dhidi yao zinapungua,” amesema.
Baadhi ya wanufaika wa mradi huo akiwemo, Leah Shibanda na Asha Noel wa Kata ya Utengule Usangu Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya walisema mafunzo waliyopewa yamegusa mahitaji halisi ya maisha yao katika kujikwamua kiuchumi huku wakiiomba serikali na wadau wanaotekeleza mradi huo kuwatafutia masoko ya mpunga kwani wanazalisha kwa wingi lakini wanauza kwa bei isiyo rafiki.
Akieleza namna baadhi ya vijana na wanawake katika eneo lake walivyonufaika, Mtendaji wa Kijiji cha Ndala wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, Anna Tenga alisema mradi huo umewasaidia kuanzisha vikundi vitano kati ya hivyo vinne ni vya wanawake na kimoja cha vijana.
“Vikundi vitatu vya wanawake na hicho kimoja cha vijana vimeshasajiliwa, kufungua akaunti na kupeleka maombi ya mkopo halmashuri, ambapo kikundi kimoja kiko kwenye hatua za kuchanga fedha kisajiliwe na kufungua akauti benki,” alisema Anna na kuongeza.
“Uanzishwaji wa vikundi hivi umetokana na uwepo wa mradi wa Mwanamke imara kwenye kata yetu ingawa serikali ya awamu ya tano ilianza kutoa mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu lakini hakuna kundi lolote lililounda vikundi ili kunufaika na fursa hiyo mimi nilipokuwa nawasihi waanzishe vikundi walidai hawana elimu ya fedha na masuala ya ujasiriamali hivyo hofu yao wakikopa watashindwa kurejesha mkopo sasa wanasubiri mkopo kwa shauku kubwa ili waendeleze biashara zao walizoanzisha baada ya kupewa elimu ya ujasiriamali na Shirika la Kwieco,” amesema.
Mratibu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAWLA, Barnabas Kaniki alisema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu ulianza Septemba mwaka 2020 utakamilika mwaka 2023 lakini kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu waanze kuutekeleza wamebaini changamoto inayovikabili vikundi ni ukosefu wa mtaji.
Alisema kutokana na changamoto hiyo mradi umetenga fedha kwa makubaliano na taasisi za fedha zitoe mikopo kwa vikundi huku akiweka wazi Kuwa jitihada mbalimbali zinaendelea ambapo benki mbili wanazoendelea kufanya nazo mazungumzo zimeonyesha nia ya kutoa Sh Milioni 200 hadi 500 kwa vikundi ambavyo vinakidhi vigezo vya kukopesheka.
“Vikundi vingine vitapata mikopo ya halamashauri mfano hapa Mbarali Mbeya kuna vikundi 10 ambavyo ni miongoni mwa vikundi tunavyofanya navyo kazi viliishapata mikopo kutoka halmashauri hivyo tunaamini mwaka huu pia vitapata, jukumu letu ni kuendelea kuvipa elimu na tunashirikiana na serikali kuwawezesha wajasiriamali kuwa na maeneo tengefu kwa ajili ya kufanyia biashara,” alieleza Kaniki.