24.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake, Vijana 3,227 wawezeshwa kiuchumi kutokomeza ukatili wa kijinsia

Na Clara Matimo, Mtanzania Digital

JITIHADA za kuwawezesha kiuchumi wanawake  na vijana nchini zinazidi kupiga hatua ambapo jumla ya wanawake na vijana 3,227 katika vikundi 300  kutoka mikoa ya Mbeya, Kilimanjaro na Njombe wamewezeshwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Makundi hayo yamewezeshwa kupitia mradi wa Mwanamke Imara wenye lengo la kutokomeza aina zote za ukatili wa kijinsia unaotekelezwa kwenye mikoa hiyo na  mashirika manne ambayo ni Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania(TAWLA), WILDAF, KWIECO na TANLAP Kwa ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).

(kushoto) wakishuhudia jinsi ambavyo baadhi ya  vijana wa kikundi cha uhunzi(kulia) kilichopo Kijiji cha Mkiu Kata ya Lubonde wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe wakiendelea na shughuli zao za uhunzi walipowatembelea hivi karibuni lengo likiwa ni kuona wanatumiaje mafunzo ya uwezeshwaji kiuchumi waliowapa. Picha na Clara Matimo.

Hayo yalielezwa hivi karibuni na Afisa Mradi  huo kutoka Shirika la Kwieco, Peter Mashingia wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mkoani Kilimanjaro waliokuwa kwenye ziara ya kuona changamoto na mafanikio ya mradi huo.

Mashingia alisema wanufaika hao wamepewa mafunzo ya usimamizi wa shughuli za ujasiriamali, ujuzi kwenye  mipango na uendelevu wa  biashara, utunzaji fedha, uanzishaji biashara,  namna ya kuimarisha ujuzi katika masuala ya  kuongeza thamani kwenye bidhaa za kilimo, ufugaji wenye tija na masuala yote ambayo yanaweza yakatafsiri ustawi wa mwanamke na kijana kwenye kufanya shughuli za ujasiriamali zenye tija.

“Tumejifunzakwamba asilimia kubwa sana ya wanawake na vijana walioimarisha vipato vyao wana nafasi  kubwa ya kupunguza utegemezi na utegemezi ukipungua miongoni mwao  kwa asilimia kubwa sana hatari za ukatili wa kiuchumi dhidi yao zinapungua,” amesema.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo akiwemo, Leah Shibanda na Asha Noel wa Kata ya Utengule Usangu  Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya  walisema mafunzo waliyopewa yamegusa mahitaji halisi ya maisha yao katika kujikwamua kiuchumi huku wakiiomba serikali na wadau wanaotekeleza mradi huo kuwatafutia masoko ya mpunga kwani wanazalisha kwa wingi lakini wanauza kwa bei isiyo rafiki.

Akieleza namna baadhi ya vijana na wanawake katika eneo lake walivyonufaika, Mtendaji wa Kijiji cha Ndala wilayani Rungwe mkoa wa Mbeya, Anna Tenga alisema mradi huo umewasaidia kuanzisha vikundi vitano kati ya hivyo vinne ni vya wanawake na kimoja cha vijana.

 “Vikundi vitatu vya wanawake na hicho kimoja cha vijana vimeshasajiliwa, kufungua akaunti na kupeleka maombi ya mkopo halmashuri, ambapo kikundi kimoja kiko kwenye hatua za kuchanga fedha kisajiliwe na kufungua akauti benki,” alisema Anna na kuongeza.

“Uanzishwaji wa vikundi hivi umetokana na uwepo wa mradi wa Mwanamke imara kwenye kata yetu ingawa serikali ya awamu ya tano ilianza kutoa mikopo kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu  lakini hakuna kundi lolote lililounda  vikundi ili kunufaika na fursa hiyo mimi nilipokuwa nawasihi waanzishe vikundi walidai hawana elimu ya fedha na masuala ya ujasiriamali hivyo hofu yao wakikopa watashindwa kurejesha mkopo sasa wanasubiri mkopo kwa shauku kubwa ili waendeleze biashara zao walizoanzisha baada ya kupewa elimu ya ujasiriamali na Shirika la Kwieco,” amesema.

Afisa Mradi wa  Mwanamke Imara kutoka Shirika lisilo la serikali linalojishughulisha na uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi na haki za binadamu (Kwieco), Peter Mashingia, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) ofisini kwake mkoani Kilimanjaro hivi karibuni  waliokuwa kwenye ziara ya kuona changamoto na mafanikio ya mradi huo. Picha na Clara Matimo.

Mratibu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini  kutoka TAWLA, Barnabas Kaniki alisema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu ulianza Septemba mwaka 2020 utakamilika mwaka 2023 lakini  kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu waanze kuutekeleza wamebaini changamoto inayovikabili vikundi ni  ukosefu wa mtaji.

Alisema kutokana na changamoto hiyo mradi umetenga fedha kwa makubaliano na taasisi za fedha zitoe mikopo kwa vikundi huku akiweka wazi Kuwa jitihada mbalimbali zinaendelea ambapo benki mbili wanazoendelea kufanya nazo mazungumzo zimeonyesha nia ya kutoa Sh Milioni 200 hadi 500 kwa vikundi ambavyo vinakidhi vigezo vya kukopesheka.

“Vikundi vingine vitapata mikopo ya halamashauri mfano hapa Mbarali Mbeya  kuna vikundi 10 ambavyo ni miongoni mwa vikundi tunavyofanya navyo kazi viliishapata mikopo kutoka halmashauri hivyo tunaamini mwaka huu pia vitapata, jukumu letu ni kuendelea kuvipa elimu na tunashirikiana na serikali kuwawezesha wajasiriamali kuwa na maeneo tengefu kwa ajili ya kufanyia biashara,” alieleza Kaniki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles