22.7 C
Dar es Salaam
Sunday, May 5, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa: Serikali za EAC kuendelea kukuza sekta ya michezo

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) zitaendelea kuchukua hatua za makusudi za kukuza michezo ndani ya jumuiya hiyo kuwa sekta ya michezo imekuwa chanzo kikubwa cha biashara, utalii, kuimarisha afya na ajira kwa vijana.

Amesema hayo leo, Desemba 06, 2021, wakati wa akifungua mashindano ya 11 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jijini Arusha.

“Nitoe wito tuendelee kutumia majukwaa ya namna hii kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha ushirikiano wetu kwa ajili ya mustakabali na manufaa makubwa ya wananchi wetu,”amesema.

Majaliwa amesema kuwa michezo hiyo lengo lake kuu ni kuimarisha mahusiano na kuifanya jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa imara zaidi.

“Majukwaa ya namna hii yamekuwa chachu ya kuleta mwamko mkubwa wa masuala ya sanaa, burudani na michezo ndani ya jumuiya,”ameeleza.

Waziri Mkuu amewasihi wabunge hao waendelee kuimarisha ushiriki wao katika suala la michezo kwani imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha afya, hivyo kusaidia kupambana na magonjwa yasiyoambukiza.

“Kwa hiyo, nitoe rai kwa Bunge la Afrika Mashariki kusimamia kwa karibu ushiriki wa michezo kwa wabunge na hata wananchi wa Jumuiya yetu,” amesema Waziri Mkuu.

Kaulimbiu ya Mashindano haya ni ‘Strengthening Integration through Inter-Parliamentary Games in the Covid-19 era’ yaani kuimarisha masuala ya mtangamano katika kipindi hiki cha Uviko-19 kupitia Mashindano ya Mabunge ya Jumuiya.

Spika wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Martin Ngoga, amesema kuwa moja ya lengo la michezo hiyo ni kujenga mshikamano wa kibunge na kuendeleza mahusiano ya kibunge katika jumuiya hiyo.

Naibu Spika wa Tanzania Dk. Tulia Ackson, amesema mashindano hayo yatasaidia kuongeza umoja kama nchi za Afrika Mashariki ambao wameamua kuwa wamoja na watapata fursa ya  kujadiliana na hatimaye kuja na mambo ambayo watashauri viongozi wa nchi zao juu ya ustawi wa wananchi.

Katibu Mkuu wa Jumuiya Afrika Mashariki Dk. Peter Mathuki, amesema kuwa michezo hiyo ni sehemu ya jitihada za jumuiya hiyo kuiunga mkono Tanzania wakati inaadhimisha miaka 60 ya Uhuru.

“Mbali na hilo mheshimiwa Waziri Mkuu nikuhakikishie kuwa Jumuiya yetu ipo imara na inakuwa kwa kasi sana na hii ni sababu ya ushirikiano tunaoupata kutoka kwa viongozi wa nchi,” amesema Dk. Mathuki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles