Na FRANCIS GODWIN, IRINGA
WAKATI Mkoa wa Iringa ukianza kampeni ya miezi sita ya upimaji wa Virusi vya Ukimwi kupitia ‘Furaha yangu pima, jitambue, ishi’, imeelezwa kuwa wanaume wengi mkoani hapa hawana tabia ya kupima Ukimwi huku wengine wakituma wake zao kwa ajili ya kupima pindi wanapokuwa wajawazito.
Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mundi, Jamhuri Willaim ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika Mwembetongwa mjini hapa.
Alisema takwimu zinaonyesha wanaume zaidi ya 18,416 ndio ambao wanatumia dawa za ARV kwa ajili ya kufubaza makali ya VVU, wakati wanawake wakiongoza kwa kutumia dawa hizo za ARV kwa kufikia wanawake 34847 kuwa takwimu hizo zinaonyesha wanaume wengi bado hawajapima kujua hali zao na kuanza matumizi ya tiba.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha wanawake ndio wanaojitokeza kupima VVU wakati wanaume wakiwa nyuma na kupitia kampeni hiyo, mkoa unakusudia kupima watu 90,000.
“Kampeni hii ya kupima VVU na kuanza kutumia tiba ya ARV mapema, tunaomba wanaume wote kujitokeza na wananchi wengine wote,” alisema DC Wiliam.
Alisema baada ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia mpango wa kitaifa wa kudhibiti Ukimwi kwa kushirikiana na TACAIDS na wadau wa USAID kuja na kampeni ya Furaha yangu mjini Dodoma, Mkoa wa Iringa nao walijipanga kwa ajili ya kampeni hiyo.
Awali Mbunge wa Viti Maalumu wa Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati (CCM), aliwataka wanawake kuwahamasisha waume zao kwenda kupima kwani kuendelea kuwatumia wanawake kupima kwa niaba yao maambukizi ya Ukimwi hayatapungua mkoani hapa.