MARTIN MAZUGWA NA MITANDAO
MCHEZO wa soka ni kati michezo iliyojikusanyia mashabiki wengi duniani kutokana na uwekezaji mkubwa uliowekwa na makampuni makubwa, ambayo yamekuwa yakiutumia kufanya matangazo yao ili kuuza bidhaa.
Kutokana na uwekezaji huo ndio chanzo cha kutoa nyota ghali zaidi duniani Neymar, ambaye amenunuliwa kwa kiasi cha Euro milioni 198 kutoka Barcelona na kuvunja rekodi ya nyota wa Manchester United Paul Pogba, aliyenunuliwa kwa kiasi cha Euro milioni 89 kutoka Juventus.
Wafuatao ni wacheza soka ghali hivi sasa katika soka la wanawake, ambalo limekuwa likipiga hatua kila kukicha.
Alexandra Morgan
Raia wa Marekani ambaye anashika nafasi ya kwanza katika orodha hii, anakusanya kiasi cha dola za Kimarekani 450,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 998,130,000 za Kitanzania, nyota huyo aliyezaliwa Julai 2 mwaka 1989 amekuwa katika ubora wa hali ya juu na kuisaidia timu yake ya Orlando Pride kubeba medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki.
Wamarekani wamekuwa wakijivunia mshambuliaji huyo, mwenye uwezo mkubwa wa kufumania nyavu, ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha California Berkeley, amekuwa akiingiza fedha hizo kutokana na matangazo anayoyafanya ya bidhaa mbali mbali.
Marta Vieira
Hakuna mpenda soka asiyetambua uwezo wa nyota Marta Vieira da Silva aliyezaliwa Februari 19, 1986. Ni nyota wa kimataifa wa Brazili anayecheza nafasi ya ushambuliaji katika klabu ya FC Rosengard ya nchini Sweden na timu ya Taifa ya Brazili, anashika nafasi ya pili katika orodha hii akiwa anaingiza kiasi cha dola za Kimarekani 400, 000 ambazo ni sawa na Sh milioni 887,226,000 za kitanzania .
Nyota huyo ambaye ameweka rekodi ya kufunga mabao mengi kwa upande wa wanawake, akipachika mabao 15 na kuvunja rekodi ya Birgit Prinz aliyekuwa na mabao 14.
Abby Wambach
Mkali huyo aliyebeba tuzo ya nyota bora wa mwaka mara sita nchini Marekani, Mary Abigail Wambach, amezaliwa Juni 2, 1980, amebeba medali mbili za dhahabu za mashindano ya Olimpiki, anashika nafasi ya tatu katika orodha hii akiwa anakusanya kiasi cha dola za Kimarekani 200000 ambazo ni sawa na Sh milioni 443,613,000 za kitanzania.
Abby pia anashikilia rekodi ya kimataifa ya kuwa mfungaji bora, aliyefunga mabao mengi zaidi kuliko mchezaji yeyote akiwa amefunga mabao 184 .
Heather Mitts
Nafasi ya nne inashikiliwa na mlinzi wa kati wa zamani wa Marekani , Heather Mitts Feeley aliyewahi kukipiga katika klabu za Philadelphia Charge, Boston Breakers, Philadelphia Independence pamoja na Atlanta Beat.
Mitts ambaye alikuwa na kipaji cha hali ya juu hadi anastaafu, alikuwa tayari amevaa medali tatu za dhahabu anaingiza kiasi cha dola za Kimarekani 150000 sawa na Sh milioni 332,710,000 za kitanzania, hivi sasa ni kocha katika kikosi cha taifa hilo.
Nicole Banecki
Nafasi ya tano inashikiliwa na nyota wa klabu ya SC Freiburg, Nicole Banecki aliyezaliwa Septemba 3, 1988 ambaye ni nyota wa kutumainiwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani, ambayo alianza kuichezea mwaka 2008 huku mchezo wake wa kwanza ukiwa dhidi ya Finland.
Nicole anaingiza kiasi cha dola la Kimarekani , 90000 sawa na Sh milioni 199,626,000 za kitanzania kutokana na kazi kubwa anayoifanya uwanjani na kuwa kipenzi cha mashabiki.
Amandine Henry
Bingwa mara mbili wa tuzo ya mchezaji bora wa FIFA na mshindi wa mpira wa shaba katika fainali za kombe la dunia mwaka 2015 raia wa Ufaransa, Amandine aliyezaliwa Septemba 28, 1989, amekuwa katika ubora wa hali ya juu miaka ya karibuni, anashika nafasi ya sita akiwa anaingiza kiasi cha dola za Kimarekani 70000 sawa na Sh milioni 155,265,000 za kitanzania.
Nilla Fischer
Nani asiyeukumbuka uwezo wa kiungo wa kati wa Sweden , Nilla Fischer aliyezaliwa Agosti 2,1984, aliuonyesha mwaka 2001 katika mchezo dhidi ya Norway, kutokana na soka lake maridadi uwezo uliosababisha apate mkataba katika kikosi cha VFL Wolfuburg.
Nyota huyo anashika nafasi ya saba katika orodha ya nyota wanaoingiza fedha nyingi, akiwa anakusanya kiasi cha dola za Kimarekani 67,500 sawa na Sh milioni 149,719,000 za kitanzania.
Hope Solo
Nyota huyo anayekipiga katika klabu ya Seattle Reign, raia wa Marekani, Hope Solo, alizaliwa Julai 30, 1981 anaingiza kiasi cha dola za Kimarekani 65000, sawa naSh milioni 144,174,000 za kitanzania, anashika nafasi ya nane katika orodha hii ya wanawake wanaoingiza kiasi kikubwa cha fedha.
Ni nyota anayelipwa kiasi kikubwa cha mshahara nchini Marekani, kutokana na uwezo mkubwa wa kucheza soka.
Jonelle Filigno
Namba tisa inashikiliwa na raia wa Canada, Jonnelle Filigo nyota aliyepata umaarufu mkubwa katika mchezo wake wa kwanza wa kulipwa kwa kufunga mabao matatu katika mchezo ulioisha kwa sare ya 3–3 dhidi ya Washington Spirit, uliopigwa Mei 21, 2014 katika dimba la Maryland Soccer Plex.
Filigno ambaye alianza kupewa nafasi katika kikosi cha timu ya taifa akiwa na umri wa miaka 17 mwaka 2008, anashika nafasi hii akiwa anaingiza kiasi cha dola za kimarekani 60000 sawa na Sh milioni 133,084,000 za kitanzania.
Laure Boulleau
Orodha hii inafungwa na raia wa Ufaransa Laure Pascale Claire Boulleau, alizaliwa Oktoba 22 1986, anakipiga kwa matajiri wa jiji la Paris, PSG na timu ya taifa ya Ufaransa, anaingiza kiasi cha dola 60000, sawa na Sh milioni 133,084,000 za kitanzania, beki huyo kisiki anaingia katika orodha hii ya kuwa nyota wanaoingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa upande wa wanawake.