21.4 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAJERUHI YANAMALIZA UWEZO WA ANDY MURRAY

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

HAKUNA kipindi kigumu kwa wanamichezo kama pale wanapopata majeruhi hasa katika michuano muhimu ya wao kuwapa nafasi ya kutetea timu zao au katika kipindi cha kuwania tuzo binafsi.

Ni bora mwanamichezo apate majeraha ya kawaida ambayo yanaweza kumfanya akawa nje ya uwanja kwa wiki chache tofauti na yule ambaye anweza kukaa nje kwa msimu mzima, akirudi atakuwa na wakati mgumu wa kurejesha kiwango chake na kufikia hatua ambayo wengine wapo.

Yupo wapi nyota wa mchezo wa Golf duniani, Tyga Woods, aliyetamba kwa kipindi kirefu kwenye mchezo huo akiwa bingwa wa michuano mbalimbali na kuongoza kwa utajiri wa wanamichezo duniani, lakini leo hii haonekani kwenye mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi ya mgongo kwa kipindi kirefu.

Mbali na kuwa na umri wa miaka 41, haimaanishi kuwa kiwango chake kimeshuka kutokana na kufanya vizuri tangu mwaka 1999 alipoanza kulitangaza jina lake kwa kutwaa tuzo kubwa ikifuatiwa mwaka 2000, 2001, 2002, 2003, 2005, 2007, 2009 na 2013, lakini baada ya hapo amekuwa kimya kutokana na kufanyiwa upasuaji wa mgongo mara kwa mara.

Leo hii nyota wa tenisi ambaye anashika nafasi ya pili kwa ubora duniani upande wa wanaume, Andy Murray, yupo hatarini kumsahau kwenye ramani ya mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na majeruhi.

Anaonekana kama hana uwezo mkubwa katika kipindi cha hivi karibuni na kuna wakati alikuwa anajaribu kucheza michuano mbalimbali huku akiwa na maumivi ili kujaribu kupigania mataji, lakini kutokana na ushindani uliopo anaonekana kuburuzwa kwa kiasi kikubwa.

Mwezi uliopita alikuwa tayari kushiriki michuano mikubwa ya tenisi nchini Marekani ambayo inajulikana kwa jina la US Open, lakini kutokana na hali yake ya kusumbuliwa na nyonga aliamua kujitoa kwenye mbio hizo.

Madaktari wake wamemshauri kukaa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu huu, hivyo ataonekana viwanjani mapema mwakani kitendo ambacho kitazidi kumshusha kwenye viwango vya mchezo huo duniani.

Safari yake kuanzia Januari mwaka huu ilikuwa ya kusuasua, hivyo wataalamu wa mchezo huo wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa nyota huyo ikawa ni safari yake kuelekea kupotea kwenye mchezo huo.

Januari- Alikuwa na wakati mgumu kwenye michuano ya Australia Open, huku akichezea kichapo kutoka kwa mipinzani wake Mischa Zverev, katika raundi ya nne ya michuano hiyo.

Machi- Aliondolewa kwenye michuano ya Miami Open nchini Marekani na kudai kwamba alikuwa anasumbuliwa na mafua, hivyo alilazimika kuikosa michuano ya Great Britain, Davis Cup hatua ya robo fainali.

Julai- Hapo alianza kuweka wazi kuwa anasumbuliwa na tatizo la nyonga kabla ya kuwania kutetea ubingwa wake wa michuano ya Wimbledon, hata hivyo hakufanya vizuri na alitupwa mapema kwenye michuano hiyo.

Agost- Nafasi yake ya bingwa namba moja kwa ubora duniani kwenye mchezo huo ulichukuliwa na Rafael Nadal kutokana na yeye kushindwa kufanya vizuri kwenye baadhi ya mashindano, hivyo akawa nafasi ya pili.

Kwa upande wake Murray anaamini kwamba ana nafasi ya kuonesha ubora wake baada ya kurudi kutoka benchi kwenye michuano ya Australia Open, mapema mwakani na kupigania nafasi yake ya kwanza.

Hata hivyo anaamini haitokuwa kazi rahisi kwa upande wake kuweza kurudi kwenye nafasi ya kwanza au kuwa bora kama ilivyo zamani kutokana na hali ya majeruhi.

“Nimeambiwa nipumzike hadi Januari mwakani, hiki ni kipindi kirefu bila ya kushiriki michuano yoyote, ninaamini wenzangu watakuwa kwenye ubora wa hali ya juu kwenye michuano ya Australia Open.

“Lakini kutokana na uzoefu wangu na uwezo nilionao ninaamini nina kila sababu ya kupambana na kufanya vizuri nikirudi kutoka majeruhi,” alisema Murray.

Hata hivyo bingwa huyo amedai kwamba kwa kipindi ambacho atakuwa nje ya uwanja atatumia muda wake kuangalia nini wenzake wanakifanya ili kuja moja kwa moja katika ushindani mwakani.

“Nahofia kufanya vibaya, lakini nitahakikisha ninawasoma wapinzani kwa kipindi hiki huku nikiwa nafanya mazoezi mepesi kwa ajili ya maandalizi ya mwakani ni wazi hali hii ya majeruhi inamaliza uwezo wangu,” aliongeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles