23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaozaa mfululizo, mapacha hatarini kuzaa njiti

mtotoNA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM

WANAWAKE wanaojifungua mfululizo katika muda mfupi wako hatarini   kuzaa watoto njiti ikilinganishwa na wanaozaa kwa mpangilio.

Vilevile, wanaozaa mapacha mara nyingi pia wana uwezekano mkubwa wa kupata mtoto njiti.

Daktari Bingwa wa Watoto Njiti wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Augustino Massawe alisema hayo jana katika maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti Duniani, yaliyofanyika hospitalini hapo.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto 10 wanaozaliwa, mmoja huwa njiti.

“Kina mama wanaozaa karibu karibu bila kuupumzisha mwili nao wana hatari ya kuzaa watoto njiti kwa vile  njia zao hufunguka mapema ikilinganishwa na wale wanaozaa kwa kuacha muda kutoka uzazi mmoja hadi mwingine.

“Lakini pia asilimia 20 ya wanaojifungua siku hizi nchini ni watoto yaani wapo chini ya umri wa miaka 18 unaoshauriwa, hawa wapo katika hatari ya kuzaa watoto njiti,” alisema.

Dk. Massawe alisema mambo yanayochangia watoto kuzaliwa kabla ya muda ni kuzorota kwa afya ya mama, umaskini,   upungufu wa damu na kuugua magonjwa kama vile malaria.

Kaimu Mkurugenzi Huduma za Upasuaji wa Muhimbili, Dk. Julieth Magandi alisema idadi ya watoto njiti imeongezeka maradufu katika miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na iliyopita.

Alisema takwimu zinaonyesha idadi hiyo imeongezeka kutoka watoto 30 mwaka 2012 hadi kufikia watoto 1,500 mwaka 2015/16, hatua hiyo inayomaanisha katika kipindi cha miaka minne pekee, limekuwapo ongezeko la watoto njiti 1,200.

“Takwimu za taifa zinaonyesha asilimia 13 ya watoto huzaliwa wakiwa na uzito pungufu ambao huchangia kwa asilimia 86 ya vifo vya watoto wachanga.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),   kila mwaka duniani huzaliwa watoto njiti milioni 15. Uzito pungufu wa kuzaliwa una madhara makubwa na huathiri ukuaji wa watoto wachanga kuishi na kukua,” alisema.

Daktari huyo alisema kuzaliwa kabla ya muda ni tatizo linalochangia vifo vya watoto wachanga kwa asilimia 27 na   vifo hivyo husababishwa na magonjwa ya vimelea vya bakteria na matatizo ya kupumua.

“Tunatumia njia ya kangaroo ambako mama humfunga mtoto kifuani pake na kukaa naye.

“Hivi karibuni tumeweza kupata dawa ya kukomaza mapafu lakini ni ghali, dozi kwa ajili ya mtoto mmoja ni Sh milioni 1.2,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles