29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kijana mrefu ahitaji mamilioni upasuaji

tallNA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM

KIJANA Baraka Elias (35), mwenye urefu wa futi 7.4 anahitaji zaidi ya Sh milioni 15  kufanikisha matibabu ya kubadilisha nyonga yake ambayo imevunjika.

Kijana huyo   alishindwa kupata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kutokana na mashine za taasisi hiyo kushindwa kuendana na urefu wake.

Matibabu yanatakiwa kufanyika nje ya nchi.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema jana kuwa  fedha hizo ni za matibabu pekee bila kujumuishwa gharama nyingine ikiwa ni pamoja na zile za usafiri, malazi na mtu atakayemsindikiza.

Kwa sasa Baraka anasubiri majibu ya madaktari kujua nchi gani ambako atapewa rufaa.

Ingawa  kijana huyo anasubiri majibu ya madaktari, imeelezwa kuwa nchi pekee ambazo zina uwezo wa kufanikisha matibabu yake kwa ufanisi   ni India na Uingereza.

“Tunavyo vifaa vya kisasa lakini urefu wake umekuwa changamoto kwa sababu  yeye ana futi 7.4 na vitanda vyetu vina futi sita.

“Gharama za kutibu tatizo alilo nalo hapa kwetu huwa zinatofautiana, kwa yeye ingemgharimu Sh milioni 15.

“Wengi huwa wanashindwa na hivyo kusaidiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na hata yeye mwenyewe alipoambiwa gharama hizo alisikitika kwa sababu  uwezo wake ni mdogo.

“Sasa kama atapata rufaa ya kwenda nje ya nchi italazimika awe na fedha hizo kufanikisha matibabu yake, kwa jinsi tunavyofahamu nchi pekee ambazo ataweza kupata matibabu ya uhakika ni India na Ujerumani,” alisema Mvungi.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, nyumbani kwa wazazi wake Mtaa wa Bwela, Pugu Magohe nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, Elias alisema alipata tatizo hilo baada ya kudondoka alipokuwa akishuka ngazi nyumbani kwake Mbinga, mkoani Ruvuma alipokuwa akiishi.

Alisema siku ya tukio, mvua ilikuwa imenyesha na   aliteleza kwenye ngazi alipokuwa akishuka kutoka ndani ya nyumba yake hiyo.

“Mimi ni mwenyeji wa Musoma, wazazi wangu wanaishi hapa Dar es Salaam, kule Ruvuma nilikuwa najishughulisha na   kilimo kidogo cha mazao ya chakula.

“Mimi ni mwinjilisti hivyo nilikuwa nafanya pia kazi za kuinjilisha watu katika Kanisa  moja la Wasabato mkoani humo,” alisema.

Alisema baada ya ajali hiyo alipelekwa katika Hospitali ya Peramiho ambako alifanyiwa kipimo cha X-rays na kuonekana   nyonga yake ilikuwa imevunjika na alielezwa matibabu hayo yanapatikana Muhimbili pekee, hivyo akapewa rufaa.

“Lakini hapa wameniambia nisubiri rufaa nyingine ya kwenda kutibiwa nje ya nchi na taarifa hiyo nimeipokea kwa mtazamo chanya. Nasubiri nijulishwe nitaenda wapi kutibiwa lakini nahitaji msaada maana sina uwezo wa fedha.

“Naomba Watanzania wenzangu wanisaidie, nipo tayari kupokea msaada wowote maana hata haya magongo ninayotembelea ni mtu aliniwezesha,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles