Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
YANGA imedhirisha kuwa msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ina jambo lake baada ya kushinda mchezo wa tatu mfululizo kwa kuichapa KMC mabao 2-0 katika mechi iliopigwa leo Oktoba 19, 2021 kwenye Uwanja wa Maji Maji, mjini Songea.
Mabao ya Wanajangwani hao yamefungwa na Fiston Mayele dakika ya tano na Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 12 na kuifanya Yanga kufikisha alama tisa na kukaa kileleni mwa ligi hiyo.
Ushindi wa leo unaonesha muelekeo wa kufanikiwa kwa mipango ya kocha wao Nasreddine Nabi  ambaye kabla ya mchezo huo alisema mikakati yake ni kushinda bao zaidi ya moja tofauti na michezo miwili iliyopita ambayo wameshinda kwa bao moja moja,pia kulinda lango lao wasiruhusu kufungwa.
Mchezo wa kwanza msimu huu, Yanga ilicheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kisha kukutana na Geita Gold dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kwa upande wa KMC, kipigo cha leo kinaifanya kuendelea kuwa mkiani ikiwa na alama moja baada ya kucheza mechi tatu, ikipoteza mbili na kutoka sare moja.
Ikumbukwe kuwa msimu uliopita Oktoba 25, 2020, KMC ambayo pia leo ilikuwa mwenyeji, ilipeleka mchezo wake na Yanga jijini Mwanza na kufungwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.