24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

DC Muleba aonya matarjiri wanaofadhili wavuvi haramu

Na Renatha Kipaka, Muleba

Watu sita kutoka kisiwa cha Bumbire kijiji Iroba, mwalo wa Mahaiga wamekamatwa wakijishughulisha na uvuvi haramu kutokana na doria iliyoendeshwa na Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji, Afisa Uvuvi wa kata kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha operesheni cha wilaya dhidi ya uvuvi haramu.

Hata hivyo watu hao wamekutwa Samaki wadogo walikuwa chini ya kiwango sentimita 48 kinachostahili kuvuliwa aina ya Sangara na nyavu haramu aina ya timba vipande 15 kila kipande kina urefu wa mita mia moja.

Kauli hiyo imetolewa baada ya kukamatwa wavuvi haramu hao na kufikishwa wilayani, Mkuu wa wilaya ya Muleba, Toba Nguvila ameagiza watuhumiwa hao kufikishwa mara moja mahakamani na kusomea mashtaka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

“Wilaya ya Muleba bado ipo kwenye operesheni ya kupambana na kuondoa uvuvi haramu. Tulipata taarifa juzi usiku kutoka kwa watoa taarifa wetu na kuagiza kikosi kazi kwa kushirikiana na watendaji wa eneo husika kwenda kufanya doria ndipo walifanikiwa kuwakamata vijana hawa. Wamekamatwa wakivua samaki walio chini ya viwango wengine hawafiki hata robo kilo. Huu ni uharibifu usiovumilika na tutaendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua mpaka watakapoacha kujihusisha na uvuvi haramu,” amesema Nguvila.

Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo kwa matajiri wanaowafadhili wavuvi hao kwenda kuvua samaki chini ya kiwango kinachostahili kuacha kazi hiyo na kwenda kutafuta kazi nyingine kwani kazi hiyo haiwezi kuwalipa na amesisitiza kuwa wakikamatwa na wao hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Nitumie nafasi hii kutoa ushauri kwenu mnaofanya biashara hii muache mara moja na kama hamna biashara ya kufanya njooni ofisini nitawashauri biashara za kufanya,” amesema Mkuu wa Wilaya.

Pia ametoa onyo kwa wataalamu wa uvuvi kutoshiriki hata katika uvuvi haramu. Na kuwataka wawe waaminifu na wazalendo.

Aidha, amesema kuwa mtaaramu yeyote ambae atajihusisha na uvuvi haramu na akibainika kuhusika kwenye uharamu huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwasababu sio jambo jema kwenye Taifa letu. Hivyo tuwe waaminifu kwa nchi yetu na ni lazma tuwe wazalendo na kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anapambana na kutimiza wajibu kwenye nafasi yake.

Kwa upande wake Afisa Uvuvi wa kijiji cha Iroba, Bamanya Deogratias ameeleza kuwa doria ya kuwakamata wavuvi hao ilifanyika kwa ushirikiano wa maafisa uvuvi pamoja na watendaji wa kata na kufanikisha kukamata mitumbwi mitatu iliyokuwa na wavuvi 6 na kukutwa na samaki waliochini ya kiwango na timba vipande 15 zenye jumla ya urefu wa mita 1500 zenye thamani ya Sh milioni 2.

Kwa upande wake Afisa Uvuvi wa Wilaya, Wilfred Tibendelana ameeleza kuwa aina ya nyavu za timba zilizokamatwa zina rangi sawa na maji hivyo samaki akiwa anatafuta chakula akiingia kwenye nyavu hizo hawezi kutoka, matokeo yake kwa siku moja nyavu hizo zinaweza kufanya uharibifu wa tani moja na nusu. Na nyavu hizo haziozi.

Watuhumiwa tayari wamefikishwa mahakamani kwa ajili ya kuendelea na hatua zingine za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles