Mwanaidi Waziri, Sumbawanga
Wakazi wa tarafa ya Mambwenkoswe wilaya ya Kalambo waishio mpakani na nchi jirani ya Zambia wameishauri serikali kupanga wasimamizi wa uchaguzi wazoefu kuepukana na uwezekano wa raia wa kigeni kushiriki kupiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na mkuu mkuu mwaka 2020.
Wananchi hao wamedai hayo baada ya tathmini ya kujiandikisha katika zoezi la uboreshwaji wa dafatari la kudumu la wapiga kura ambapo kuna baadhi ya raia wa Zambia walikamatwa wakitaka kujiandikisha kwenye daftari hilo.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kalembe Michael Mengo, amesema wakati zoezi hilo likiendelea walibaini uwepo wa raia hao kigeni wakiwa katika foleni na ndipo walitoa taarifa kwa Ofisa Tarafa ya Mambenkoswe ambaye alikuja na kuwakamata kisha kuwahoji na wakakiri kuwa si raia.
“Tatizo la kujipenyeza kwa wageni hao linatokana na maofisa wanaopangwa kuandikisha au kusimamia upigaji kura kutokuwa wakazi wa maeneo hayo, hivyo inakuwa kwao kwa kuwa watu wa nchi zote mbili wa maeneo hayo wanazungumza lugha moja na utamaduni unaoshabihiana.
“Unakuta kuna Mtanzania kaoa mke wa Zambia na mwanamke huyo anaweza kushiriki zoezi la uchaguzi japokuwa hafahamu miongozo ya kisiasa ya Tanzania, hivyo ni lazima atachagua mtu kwa sura yake tu na si sifa kwa kiongozi huyo, hivyo ni lazima serikali ichukue tahadhari,” amesema Mengo.
Kwa upande wake Ofisa Tarafa wa Tarafa ya Mambwenkoswe, Mpapalika Mfaume aliwatahadharisha wananchi wa eneo hilo kuwa makini na vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga uchaguzi.