Na Safina Sarwatt-MOSHI
WANANCHI wa vijiji vya Mikocheni na Chemchem, Kata ya Arusha Chini wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, wamekimbia makazi yao baada ya kuzingirwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko.
Pia wameeleza hofu yao ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko yakiwamo ya matumbo na corona kutokana na kuwekwa kwenye eneo la shule ambapo kuna msongamano.
Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, wananchi hao wameomba msaada wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona kutokana na kuishi kwenye msongamano wa watu.
Inaelezwa kuwa hadi sasa mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Ally Rajabu, amepoteza maisha huku kaya zaidi ya 500 zikikikosa makazi kutokana na nyumba zao kuzingirwa na maji yanayotiririka kutoka Mto Kikuletwa, Ronga, Bwawa la Maji ya Kiwanda cha Sukari TPC Moshi kuvunja kingo zake na kuelekeza maji kwenye Kijiji cha Mikocheni.
Mmoja wa waathirika wa mafuriko hayo, Vicent Kalonga alisema kuwa kwa sasa wana hali mbaya kutokana kwamba hawana makazi, nyumba zao zimebomoka, mifugo imechukuliwa na maji pamoja na chakula.
“Hali ni mbaya, tunahofia usalama wa afya zetu kwani hatuna vifaa vya kujikinga na corona, hatuna chakula, tunaomba Serikali itusaidie mahali pa kuishi pamoja na vifaa vya kujikinga na chakula,” alisema Kalonga.
Diwani wa Kata ya Arusha Chini, Roger Mmary, alisema kuwa hayo ni maafa makubwa na kwamba hayaijawahi kutokea tangu miaka ya 1970.
Mmary alisema kuwa kwa sasa wananchi hao wamehifadhiwa katika majengo ya msingi Mikocheni, msikiti na kanisani.
Alisema kuwa kaya zaidi 2,700 katika vijiji viwili vya Mikocheni na Chemchem zimeathiriwa na mafuriko na kwamba kwa sasa hakufikiki hivyo huku akiiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia wananchi hao ambao kwa sasa wamehifadhiwa kwenye mashule na makanisani.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mikocheni, Evarist Komba alisema jumla vitongoji vinne vimeathirika na kwamba hali kwa sasa ni mbaya kutokana na nyumba zilizokuwa zimesalia kuendelea kuanguka na maji yanazidi kuongezeka.