26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 2, 2023

Contact us: [email protected]

Baadhi ya nchi zaanza kulegeza masharti kukabili virusi corona

WELLINGTON, NEW ZEALAND

 BAADHI ya mataifa duniani yameanza kulegeza masharti yaliyowekwa ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona, na sasa yanalenga kushughulikia uchumi ulioathiriwa. 

Nchi kadhaa zilizokuwa zimeathirika zaidi na janga hilo juzi ziliripoti kupungua kwa idadi ya vifo vya kila siku.

Italia, Hispania na Uingereza zimesema kiwango cha vifo kimeshuka chini kabisa kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Nchini Hispania, watoto waliruhusiwa kutembea mitaani kwa mara ya kwanza tangu amri ya kutotembea nje ilipowekwa wiki sita zilizopita.

 Nchi nyingi za Ulaya zinafungua viwanda pamoja na maeneo ya ujenzi. 

Nchini New Zealand, watu wataweza kununua vyakula vya kubeba kutoka katika migahawa ambayo ilipangwa kuanza kufunguliwa usiku wa jana. 

Hata hivyo, baadhi ya watu wana wasiwasi kwamba kuanza kulegeza masharti hayo mapema, kunaweza kusababisha virusi vya corona kuanza tena kusambaa kwa kasi. 

Jumla ya watu milioni 2.97 duniani kote wameambukizwa virusi hivyo. 

Idadi ya waliokufa kutokana na ugonjwa huo wa Covid-19 kwa mujibu wa majumuisho ya takwimu uliofanywa na shirika la habari la Reuters ni 205,948.

Migahawa yafunguliwa Kenya 

Waziri wa Afya nchini Kenya, Mutahi Kagwe ametangaza watu wanane zaidi wameambukizwa virusi vya corona nchini humo na pia kulegeza masharti kwenye migahawa inayouza chakula.

Tangu mara ya kwanza kutangazwa kwa virusi hivyo, jumla ya walioambukizwa nchini Kenya imefikia 363.

Aidha watu nane pia wamethibitishwa kupona na kufikisha jumla ya waliopona kuwa 114.

Wote walioambukizwa hawana historia ya kusafiri ya nje ya nchi hali inayoashiri kwamba bado kungali kuna maambukizi ya ndani kwa ndani nchini humo.

Wizara ya afya imesema kuwa itaruhusu migahawa kuanza kufunguliwa kuanzia saa 11 asubuhi na kufungwa saa 10 jioni.

Watakaoingia kuhudumiwa watahitajika kufuata utaratibu uliopo wa kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono na kuvaa barakoa kama kawaida. 

Hatua ya kutokaribiana itaendelea kutekelezwa umbali wa mita moja baina ya mtu mmoja hadi mwengine.

Lakini watakaoruhusiwa kutoa huduma ni wale watakaokuwa wamepimwa pekee.

Pia kulingana na wizara ya afya, katika migahawa hiyo, huduma ya kujiwekea chakula bado imesitishwa.

Wizara hiyo imetoa agizo la watu wote wanaoingia migahawani kupimwa kiwango cha joto na kuruhusiwa tu kuingia ikiwa litakuwa chini ya nyuzi 37.5 na mgahawa husika kuarifu wizara mara moja kuhusu mtu atakayepatikana akiwa na kiwango cha juu zaidi ya hicho ili kupata mwongozo zaidi.

Kagwe amewataka raia wote wa Kenya kuendeleza nidhamu na kuchukua jukumu wao wenyewe binafsi katika juhudi za kukabiliana na janga hili.

“Hali ya Kenya itabadilika kwa sababu yako wewe. Ikiwa tutachukua jukumu kama watu binafsi, bila shaka tutakabiliana na virusi hivi,” alisema Kagwe.

Waziri pia aligusia kwamba sasa Wakenya wameanza kutekeleza sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali upande wa usafi.

“Visa vya matatizo ya tumbo vimepungua tena pakubwa, visa vya kuharisha vimepungua,” alisema Kagwe.

Katika kukabiliana na ugonjwa wa covid-19, serikali imeunda kamati 5 za kimkakati kutoa mwongozo wa njia zitakazofanikisha Kenya kushinda vita hii. 

Hivi karibuni Rais Uhuru Kenyatta aliongeza muda wa marufuku ya watu kusafiri na kuingia au kutoka katika mji wa Nairobi na miji mingine minne (Kilifi, Kwale na Mombasa) kwa muda wa siku 21.

Pia aliongeza tena muda wa amri ya kutotoka nje kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi na moja alfajiri kwa siku 21 zaidi.

Wakati huo huo, ndege kutoka nchi za kigeni zimeendelea kupigwa marufuku kuingia Kenya kwa siku 30 zaidi.

Hivi karibuni idadi ya maambukizi imekuwa ikiendelea kuongezeka katika kaunti ya Mombasa.

Wizara ya afya nchini humo ilitangaza kwamba inatengeneza barakoa ambazo zitasambazwa kwa wananchi hivi karibuni.

Kwamba watakaofariki dunia kutokana na virusi vya corona watazikwa ndani ya saa 24, huku watu wa karibu wa familia wasiozidi 15 wataruhusiwa kuhudhuria mazishi hayo yatakayoandaliwa na Serikali.

NEW ZEALAND YARUHUSU SHULE, BIASHARA KUFUNGULIWA

New Zealand imelegeza amri kali iliyokuwa imeiweka wakati huu wa janga la virusi vya corona baada ya jana kuruhusu baadhi ya shule na biashara kufunguliwa tena.

Kulegezwa kwa masharti hayo kutaruhusu watu 400,000 kurejea makazini.

Serikali jana imeripoti kuwapo maambukizi matano mapya tu na Waziri Mkuu Jacinda Ardern amesema mamlaka husika zitaendelea kufuatilia maambukizi yoyote yale mapya. 

New Zealand ina maambukizi 1,100 yaliyothibitishwa kwa vipimo na vifo 19.

 “Hakuna maambukizi yaliyoenea na kushindwa kutambuliwa katika jamii nchini New Zealand… Tumeshinda vita hiyo,” alisema Ardern.

Ni kipindi cha mwezi mmoja tangu New Zealand ilipowataka watu kutotoka majumbani na kuamuru shughuli zote ambazo siyo muhimu kufungwa.

Ardern alisema ni mapema kusema lini nchi hiyo itafikia kuwa haina maambukizi ya Covid-19, hatua ambayo ni muhimu kuweza kufungua tena kikamilifu shughuli zote nchini.

MKAKATI WA AUSTRALIA

Sehemu ya mkakati wa kufungua tena shughuli kama kawaida katika nchi ya Australia ni kupitia matumizi ya simu za kisasa zenye app ambayo kusudio lake ni kusaidia Serikali za majimbo na wafanyakazi wa afya kufuatilia mawasiliano ya karibu na watu wengine ya wale ambao wamepimwa na kuthibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Ufuatiliaji huo unasaidia mamlaka husika kufahamu nani anatakiwa ajitenge yeye mwenyewe na nani atahitaji kuchukuliwa vipimo ili kuzuia kueneza ugonjwa huo.

Waziri wa Afya, Greg Hunt alisema jana kuwa takriban wananchi wa Australia milioni 2 walikuwa wamepakua app hiyo katika simu zao za kisasa.

BORIS JOHNSON ARUDI KAZINI

Uingereza jana ilimkaribisha Waziri Mkuu Boris Johnson kazini baada ya kuwa kiongozi wa kwanza wa dunia kuambukizwa Covid-19 na kuwekwa siku kadhaa katika wodi ya wagonjwa mahtuti.

Akizungumza nje ya Ofisi ya Downing Street, Johnson alisema kuwa anafahamu watu hawana uvumilivu tena na wana wasiwasi, lakini kulegeza masharti hivi sasa itahatarisha wimbi jipya la vifo na ugonjwa huo hali itakayoathiri zaidi uchumi.

Johnson alisema Uingereza inaendelea kubadilisha mawimbi au hali katika vita vyake vya kudhibiti virusi vya corona, lakini maelekezo ya watu kukaa mbalimbali au kujitenga ni sharti yaendelee kufuatwa, ili kuepusha uwezekano wa wimbi la pili la maambukizo. 

Johnson aliwahimiza Waingereza kutotupilia mbali juhudi zote ambazo zimefanywa hivyo kujiweka katika hatari, kwa kuyalegeza masharti mapema. 

“Sitaki kupoteza juhudi yote na kujitolea kote kulikofanywa na watu wa Uingereza na kuhatarisha kuwepo kwa mlipuko mwingine mkubwa na hasara kubwa ya watu kufa na mifumo ya afya ya taifa kuelemewa.

“Nataka mdhibiti hamasa zenu, kwa sababu naamini hivi sasa tunakaribia kufikia mwisho wa awamu ya kwanza ya janga hili. Na japokuwa tumekabiliwa na matezo yote haya, lakini tunakaribia kufikia mafanikio.

UFARANSA KUPIGA KURA BUNGENI

Nchini Ufaransa, Waziri Mkuu Edouard Philippe anatarajiwa kuwasilisha mkakati wake wa kitaifa baada ya kulegeza masharti yaliyowekwa. 

Ofisi yake imeliambia shirika la habari la AFP kuwa baadaye, tangazo hilo katika Bunge la taifa, litajadiliwa na kisha kupigiwa kura.

ITALIA KURUHUSIWA KUTEMBELEANA

Waziri Mkuu wa Italia, Giuseppe Conte amesema watu wataruhusiwa kutembelea ndugu zao katika makundi madogo, lakini itawalazimu wavae barakoa. 

Viwanja vya umma vimepangwa kufunguliwa, lakini shule zitaendelea kufungwa hadi Septemba.

Conte alisema hakuna uamuzi uliofikiwa kuhusu lini ligi ya soka ya Serie A itarudi, lakini mchezaji mmoja mmoja anaweza kuanza mazoezi kuanzia Mei 4 na timu zinaweza kukusanyika kwa mazoezi ya pamoja Mei 18. 

Covid-19 imeua takriban watu 27,000 nchini Italia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,405FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles