25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Meatu, Bariadi waipongeza Serikali kutimiza ahadi ya maji

Na Samwel Mwanga,Simiyu

WANANCHI wa Wilaya za Meatu na Bariadi mkoani Simiyu wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi yake ya kuwapatia huduma ya maji safi na salama na kumaliza tatizo  la miaka mingi la wananchi hao kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa salama  kwa matumizi yao.

Tenki lenye kuhifadhi maji lililoko kwenye kijiji cha Gambosi wilaya ya Bariadi mkoa wa Simiyu limejengwa na Ruwasa kwa lengo la kuwapatia wananchi wa kijiji hicho huduma ya maji safi na salama.

Wananchi hao wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari waliotembelea baadhi ya miradi ya maji inayotekelezwa katika wilaya hizo kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA).

Wamesema kufikishwa kwa maji ya bomba katika makazi yao imesaidia sana kumaliza changamoto hiyo iliyowatesa kwa muda mrefu na ambayo ilikwamisha kushindwa kushiriki kazi za kiuchumi.

Miongoni mwa wananchi hao ni Minza Dwashi mkazi wa kijiji cha Gambosihi kilichoko wilayani Bariadi ambapo amesema kuwa wanawake wa kijiji hicho ndio walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo la ukosefu wa maji safi na salama kwa kuwa walilazimika kuamka mapema alfajiri kati ya saa 10 na 11 kwenda kusaka huduma ya maji huku wakipambana na wanyama wakali wakiwemo fisi.

Nae, Lucy Kulwa mkazi wa kijiji cha Mwabuzo katika wilaya ya Meatu amesema baadhi ya wanawake katika kijiji hicho ndoa zao zimevunjika kwa sababu ya kutumia muda mrefu pindi wanapokwenda kutafuta maji ambayo yanapatikana kwenye visima vya asili na kushindwa kurudi haraka nyumbani kutokana na  umbali na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.

Pia amesema kero ya maji imesababisha umaskini mkubwa,kwa kuwa wakati mwingine wanakosa muda wa kufanya kazi mbalimbali za maendeleo, badala yake wanatumia muda huo kutafuta maji.

Nkamba Sita mkazi wa kijiji cha Sangaitinje wilaya ya Meatu amesema kabla ya kufika kwa mradi huo walikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo magonjwa ya matumbo na kuhara kwa sababu ya kutumia maji ambayo sio safi na salama.

Amesema baada ya kukamilika kwa mradi sasa wamepata faraja na matumaini makubwa kwani tangu ulipoanza kufanya kazi umemaliza kabisa tatizo la maji safi na salama ambapo  sasa wananchi wanapata fursa ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.

 Muuguzi wa Zahanati ya Sangaitinje, Josephine John amesema kabla ya kujengwa kwa mradi wa maji safi na salama,changamoto kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho ilikuwa  magonjwa ya kuhara na matumbo mara kwa mara kutokana na kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa salama.

Kwa mujibu wake, sasa idadi ya watu wanaofika katika zahanati hiyo kwa ajili ya kupata matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradi hayo imepungua  kwa kiwango kikubwa.

Amewashauri wananchi wa kijiji hicho, kuendelea kutumia maji ya bomba ambayo ni  safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku, badala ya kuendelea kutumia maji ya visima vya asili.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Meatu,Mhandisi George Masawe amesema kuwa kwa sasa Serikali imekuwa ikiwapatia fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya maji na kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji katika wilaya hiyo katika maeneo ya vijijini umefikia asilimia 67.

Nae Meneja wa Ruwasa wilaya ya Bariadi, Mapengu Gendai amesema kwa sasa wamejipanga kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani kwa kuwaunganishia maji majumbani ili kutimiza ule usemi wa Ruwasa maji bombani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles