Na Ramadhan Hassan,Dodoma
WIZARA ya Fedha na Mipango imewataka wanamipango nchini kuhakikisha wanapanga na kusimamia vema utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kutekeleza na kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo ya ukosefu wa ajira.
Hayo yameelezwa leo Desemba Mosi,2021 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango,Adolf Ndunguru wakati akifungua kongamano la wanamipango la mwaka 2021 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Emmanuel Tutuba.
Ndunguru amesema kuna changamoto mbalimbali kama ukosefu wa ajira kwa vijana,athari za mabadiliko ya tabia nchi,umaskini na maradhi mapya ya UVICO 19.
“Kama wanamipango tunajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa tunapanga na kusimamia vema utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa kuweka na kutekeleza vipaumbele vya kutatua changamoto hizo,”amesema.
Ndunguru ametoa rai kwa wanamipango wasichoke kutoa ushauri na mapendekezo kwa Serikali kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu ya msingi na kuendeleza kada ya wanamipango.
“Natoa rai kwa wanamipango wote popote walipo kuendelea kuenzi nia njema ya Serikali kwa kufanya kazi kwa bidii weledi na uadilifu mkubwa,”amesema.
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema wizara inaahidi kuyafanyia kazi maazimio yote ambayo watakubaliana huku akiwasihi kuwa mabalozi wazuri wa kongamano hilo.
“Dhima ya kongamano hili ni ‘Mwanamipango Imara kwa Ustawi wa Taifa’ dhima hii imezingatia jukumu kubwa lililo mbele yetu la kuibua, kupanga, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango ya maendeleo,”amesema.
Akimkaribisha mgeni rasmi,Kamishna Msaidizi Idara ya Mipango ya Kitaifa,Wizara ya Fedha na Mipango,Ekingo Magembe amesema wanamipango wanajukumu la kuandika maandiko mazuri ambayo yatasaidia nchi kuweza kupata maendeleo.
“Tukiwa katika mchakato wa kuandaa dira ya 2025 ni lazima muongezewe uwezo wa namna bora ya kuandika maandiko pamoja na namna ya kuwa bora,”amesema.