25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaharakati Z’bar walilia mashine ya DNA

dnaNa Muhammed Khamis (UoI) -Zanzibar

WAKATI leo dunia ikiadhimisha siku ya mtoto wa kike, wanaharakati wa kutetea haki za watoto wameihoji Serikali ya Zanzibar kushindwa kuwa na mashine ya kuchunguza Vinasaba (DNA) kwa zaidi ya miaka 15 sasa.

Hayo yameelezwa katika kongamano la siku moja la kupinga udhalilishaji wa watoto lililoandaliwa na taasisi za wanaharakati hao wakiwemo Save the Children, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) lililofanyika jana mjini Unguja.

Mwanaharakati kutoka Zafela, Fatma Gharib, alisema ni muda mrefu sasa tokea walivyoanza kupiga kelele kutaka Serikali inunue mashine hiyo lakini jambo la kushangaza hadi sasa hakuna mashine hiyo na wala Serikali haijasema itapatikana kwa muda gani.

“Tunataka tupatiwe majibu sahihi mashinde hiyo ya DNA inagharimu kiasi gani cha fedha hata Serikali ishindwe kuiagiza maana hizi kelele za kutaka mashine hiyo ni miaka 20 sasa tunapiga kelele hizi, Serikali kweli haina uwezo au vipi,” alisema Fatma.

Alisema suala la kupatikana mashine ya DNA Zanzibar linahitaji dhamira ya kweli na inapaswa kushughulikiwa haraka ili kesi za ubakaji na unyanyasaji wa watoto ziweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka mahakamani badala ya kesi hizo kucheleweshwa kwa kisingizio cha kukosekana vipimo vya DNA.

“Kwa hali hii hatuwezi kupiga hatua kama hatujawa na dhamira ya dhati na ya kweli ndani ya nafasi zetu, kesi zinachelewa kwa sababu mtoto anapobakwa kunahitajika vipimo vya DNA lakini hadi watu wende Dar es Salaam na wavisubiri virudi, kwa kweli hili ni tatizo na Serikali lazima izingatie kwa kina suala hili,” alisema.

Kwa upande wake Ofisa Afya, Mwandiwe Makame Kali, alisema kusiwepo na muda wa kupoteza katika suala la kupatikana kwa mashine ya DNA kwa kuwa hakuna asiyeelewa kwamba kifaa hicho ni muhimu katika ustawi wa watoto wenye kudhalilishwa.

“Kama Serikali wameshindwa kununua basi wanaharakati wao wenyewe wafanye juhudi za kupatikana mashine ya DNA kwa sababu kisingizio kikubwa cha kuchelewa kesi za udhalilishaji mahakamani ni kukosekana kwa ripoti za DNA,” alisema Mwandiwe.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi katika kongamano hilo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Magharibi Unguja, Suleiman Khamis Juma, alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupatikana mashine ya DNA hapa Zanzibar kwani kesi nyingi zinachelewa kutokana na kukosekana ushahidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles