24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafunzi 5,000 hawajaonekana shuleni Musoma

Mwandishi Wetu

WATOTO zaidi ya 5,000 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza  mwaka huu katika Wilaya ya Musoma mkoani Mara, wameshindwa kuripoti shuleni ndani ya wiki moja toka shule zimefunguliwa.

Kufuatia hali hiyo, uongozi wa Wilaya ya Musoma, imeaangaza vita na wazazi ambao watoto wao hawajaripoti shuleni  licha ya kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk. Vicent Naano, alisema ifikapo Ijumaa ijayo mzazi ambaye hatampeleka mtoto wake shule, atafikishwa Mahakamani ili kukabiliana na mkono wa sheria.

Naano alisema katika halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini watoto 3,480 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakinin hadi Ijumaa wiki hii wanafunzi 684 tu ndio waliokuwa wameripoti shuleni.

Alisema katika Manispaa ya Musoma watoto 3,748 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini ni wanafunzi 951 tu ndio waliokuwa wamesajiliwa shuleni hadi kufikia Ijumaa.

Alisema Serikali haiwezi kuvumilia hali hiyo hasa ikizingatiwa hivi sasa wazazi wamepunguziwa mzigo wa kusomesha kwa kiasi kikubwa kutokana na sera ya elimu bure hivyo wazazi wanalo jukumu la kuhakikisha kila mtoto anapelekwa shule.

Aliwaagiza wazazi wa kuhakikisha kuwa wanawapeleka watoto wao shuleni kabla ya ijumaa ijayo na kwamba hata kama hawana sare za shule watapokelewa tu ili waweze  kuendelea na masomo ambayo yalianza tangu Januari 6.

Alisema ingawa kulikuwepo na upungufu wa madarasa katika wilaya hiyo Serikali imejitahidi kutafuta namna ambavyo wanafunzi waliofaulu wanaanza masomo kwa pamoja.

Alisema katika mikakati hiyo pamoja na mambo mengine waliamua kutumia vyumba vya maabara kama madarasa lakini cha ajabu wanafunzi walioripoti shuleni ni chini ya asilimia 20.

Alitolea mfano shule ya Sekondari ya Mugango ambapo ni wanafunzi 37 tu walioripoti shuleni hapo kati ya 320 waliochaguliwa kujiunga na shule hiyo.

Kuhusu vyumba vya madarasa, alisema jumla ya madarasa 36 yanajengwa katika wilaya hiyo ambapo yatakamilika kabla ya Februari 15.

Pia alisema wapo katika mchakato wa kufungua shule mbili za sekondari katika wilaya  hiyo ikiwa ni sehemu ya kupambana na upungufu wa madarasa na baada ya kufunguliwa shule hizo pamoja na madarasa hayo 36 kukamilika tatizo la upungufu wa madarasa litakuwa limemalizika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles