Na UPENDO MOSHA-MOSHI
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi, imewahukumu washtakiwa watano kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa Mfanyabishara wa Madini ya Tanzanite, Bilionea Erasto Msuya.
Pia, mahakama hiyo imemwachia huru mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Shwahibu Jumanne (maarufu kwa jina la Mredi), baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo na Jaji Salma Maghimbi aliyekuwa akiisikiliza.
Kwa mujibu wa Jaji Maghimbi, ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka dhidi ya washtakiwa hao watano, ulidhihirisha washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama ya kumuua kwa makusudi Bilionea Msuya.
Katika hukumu hiyo, washtakiwa waliotiwa hatiani na kuhukumia kifo ni mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mshitakiwa wa tatu, Musa Mangu, mshitakiwa wa tano, Karimu Kihundwa, mshtakiwa wa sita, Sadiki Jabir na mshtakiwa wa saba, Ally Majeshi.
“Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa dhidi yenu kwamba kwa pamoja mlikula njama na kufanya nia ovu ya kumuua mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Erasto Msuya.
“Kwa hiyo, ninawatia hatiani na kuwahukumu wote kunyongwa hadi kufa lakini mnayo haki ya kukata rufaa.
“Pia, mahakama inamwachia huru mshtakiwa wa pili, Shahibu Athumani, kwa sababu kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, hakukuwa na ushahidi wa kumtia hatiani na kumuunganisha katika kesi hii ya mauaji,” alisema Jaji Maghimbi alipokuwa akisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya saa moja.
Wakati jaji akianza kusoma hukumu hiyo, alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 27 na vielelezo 26 vya maandishi na vitu vingine huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wanane na vielelezo vinne vya maandishi.
Inaendelea…………… Jipatie nakala ya Gazeti La Mtanzania