KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amesema hadi sasa watuhumiwa wa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha walioandika barua za kukiri makosa kuomba radhi, ni zaidi ya 700 huku wengine 138 wameshaachiwa huru.
Alitoa kauli hiyo jana akiwa mjini Mpanda alipokuwa akihitimisha ziara yake ya siku tisa kwenye mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi.
Septemba 22 mwaka huu akiwa Ikulu, Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kuwaapisha viongozi aliowateua, Rais Magufuli alishauri mahabusu wa makosa mbalimbali, hasa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambao wapo tayari kuomba msamaha na kurudisha fedha walizotakatisha, wasikilizwe ndani ya siku saba.
Septemba 30, mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga, akitoa taarifa ya utekelezaji wa ushauri wa Rais Magufuli, alisema watuhumiwa 467 walijitokeza kuomba msamaha, kukiri makosa na kurejesha zaidi ya Sh bilioni 107.
Mganga aliomba kuongezewa siku tatu ili watuhumiwa walioshindwa kuandika barua kwa sababu yoyote ile wafanye hivyo, hata hivyo Rais Magufuli aliongeza siku saba.
HATUA YA SASA
Jana Rais Magufuli akizungumzia hatua iliyofikiwa kutokana na ushauri wake huo, alisema; “leo (jana) nilikuwa naongea na DPP, ameniambia mpaka leo (jana) watu 138 waliokiri kutakatisha fedha wametoka, wamesharudisha baadhi ya mabilioni ya fedha na wako huru, wameenda kujumuika na familia zao.
“Sisi tulitoa msamaha na tunamshukumu Mungu aliyewagusa wao na kutubu makosa yao na kuomba msamaha, hawa sasa ni raia wema, wahesabike ni raia wema katika nchi yetu.
“Ninafahamu kwamba wapo wengine ambao walishajitokeza kuomba msamaha, wapo karibu 700, hao wengine 500 na kitu ambao bado ‘document’ (nyaraka zao) zao zinachambuliwa, nao wataendelea kuachiwa hivyo hivyo kadiri watakavyokuwa wanarudisha fedha,” alisema Rais Magufuli.
MABILIONI YALIYOLIPWA NA NYUMBA ZILIZOTAIFISHWA
Katika hatua nyingine, Serikali kupitia DPP, imeingiza zaidi ya Sh bilioni 3.6 na nyumba sita za washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kutaifisha ndani ya wiki moja.
Hayo yamebainika kutokana na idadi ya watuhumiwa waliokiri makosa Oktoba 4, 7 na 11 mwaka huu.
Oktoba 4, mshtakiwa Yasin Katera aliyekuwa akishtakiwa pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Takukuru, Godfrey Gugai, alilipa faini ya Sh milioni 100 na Serikali ikataifisha nyumba moja iliyopo Nyegezi, Mwanza.
Mfanyabiashara Magdalena Uhwello na Halima Nsubuga walikiri makosa ya kutakatisha fedha wakahukumiwa kulipa faini ya Sh milioni 101 na fedha zao dola za Marekani 388,000 kutaifishwa na Serikali.
Oktoba 7-11, wafanyabiashara watatu; Mohammed Yusufali, Arifali Paliwalla na Sameer Khan walilipa fidia Sh 1,201,000,000 baada ya kukiri makosa yao na nyumba nne zilizopo Bagamoyo na Masaki zilitaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama Kuu Kitengo cha Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Elinaza Luvanda.
DPP aliwapunguzia mashtaka kutoka 544 na kubakia mashtaka matatu.
Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya alidai shtaka la kwanza na la pili yanamkabili mshtakiwa Yusufali pekee.
Kwamba katika vipindi tofauti kati ya Januari 2008 na Januari 2016 jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Farm Plant Limited, kwa nia ya kukwepa kodi aliwasilisha ‘retuns’ za kughushi kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusababisha ukwepaji wa kodi wa zaidi ya Sh bilioni 21.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2015 hadi Januari mwaka 2016, kwa vitendo kama hivyo, mshtakiwa huyo alisababisha ukwepaji wa kodi wa Sh 1,684,559,546.47.
Shtaka la tatu la washtakiwa wote, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 2008 hadi Januari mwaka 2016 kwa vitendo vyao vya uwasilishwaji wa nyaraka za uongo za ulipaji kodi, waliisababishia TRA hasara ya Sh 24,303,777,426.70.
Mahakama iliamuru mshtakiwa Yusufali alipe fidia ya hasara aliyoisababishia TRA ya zaidi ya Sh bilioni 24 na tayari alishalipa sh bilioni moja.
Tibabyekomya alisema kiasi kilichobaki kitalipwa kwa muda wa miezi 24 ambapo kila mwezi atalipa sh 970, 990,726.08 pamoja na kutaifishwa kwa nyumba nne zilizo maeneo ya Masaki, Dar es Salaam na Bagamoyo kuwa mali ya Serikali.
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, wakili huyo aliomba alipe fidia ya Sh milioni 10 ya hasara aliyoisababishia TRA na tayari alishalipa sh milioni moja.
Alisema kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 12 kwa kila mwezi Sh 750,000.
Kwa upande wa mshtakiwa wa tatu, wakili huyo aliomba alipe fidia ya sh milioni 300 kutokana na hasara aliyoisababishia TRA na tayari alishalipa Sh milioni 200.
Tibabyekomya alisema kwa mujibu wa makubaliano, kiasi kilichobaki kitalipwa kwa kipindi cha miezi 10 kuanzia tarehe aliyoingia makubaliano na kila mwezi atalipa Sh milioni 10.
Pia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimwachia huru Mkurugenzi Mkuu wa Benki M (Tanzania), Sanjeev Kumar (63) na kumtaka kulipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 6 na faini ya Sh milioni 2 baada ya kukiri.
Kumar ametakiwa kuilipa fidia hiyo ndani ya miezi 24 na hadi sasa tayari ameshalipa Sh milioni 690.
Akisoma adhabu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema kuwa katika mashtaka mawili mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 1 kwa kila kosa.
Alisema pia mshtakiwa atatakiwa kulipa fidia ya Sh 6,039,103,579 ambazo atalipa kwa miezi 24, kwa kila mwezi atalipa Sh milioni 222.8.
Naye aliyekuwa Makamu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura, alikiri makosa ya kujipatia Sh milioni 100.9 na wakakubaliana na DPP kurejesha fedha hizo ndani kwa awamu tano hadi Septemba 30, 2020 na tayari Oktoba 7 alirejesha Sh 20,249,531.
Wakili maarufu, Dk. Ringo Tenga na wakurugenzi wenzake nao wameachiwa huru baada ya kuingia makubaliano na DPP ya kulipa Dola za Marekani 3,748,751.19 ndani ya miezi sita, kuiachia Serikali nyumba iliyopo Mikocheni, Dar es Salaam na mshtakiwa wa sita kulipa Sh milioni 30.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi alisema makubaliano mengine ambayo mahakama inatakiwa kuzingatia ni kwamba washtakiwa wamelipa Sh milioni 150, dola za Marekani 150,000 na dola 3,585,115 zilizobakia washtakiwa kuanzia wa kwanza hadi wa tano watalipa ndani ya miezi sita kuanzia Oktoba 7.
Naye mshtakiwa Frank Mwalongo alilipa Sh milioni 35 alizokubali kulipa kama fidia na faini.