31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Rugemalira awasha moto mpya sakata la Escrow

MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

IWAPO Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga atakubaliana na maombi ya Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira ya kumwachia huru ili washirikiane kupata Sh trilioni 37 nyingine mbali na zile zaidi ya bilioni 300 zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow, huenda yakafumka mambo mengine makubwa.

Takribani siku tatu zilizopita, ilielezwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa Rugemalira amemwandikia  barua DPP, akimwomba amwachie huru ili washirikiane kupata Sh trilioni 37 anazoidai Benki ya Standard Chartered ambazo Serikali itapata kodi zaidi ya Sh trilioni 6.

Aidha katika barua hiyo, Rugemalira anataka majina ya watu ambao hawakutajwa, wanaodaiwa kusomba fedha katika magunia na sandarusi kutoka akaunti ya Pan Africa Power Solution Tanzania Limited (PAP) kuwekwa wazi.

PAP ndiye mnunuzi mpya wa mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa baada ya kutokea mzozo wa malipo baina ya IPTL na Tanesco.

Sakata hilo ambalo liliibuka mwaka 2014 baada ya Sh bilioni 306 kuchukuliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika Akaunti ya Escrow, na waliochota fedha hizo kutoka Makao Makuu ya Benki ya Stanbic yaliyopo Kinondoni, Dar es Salaam hadi sasa hawajakamatwa.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (PAC), iliyochunguza sakata hilo ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alithibitisha bungeni jinsi fedha hizo zilivyochukuliwa Stanbic kwa kutumia viroba na magunia.

Sakata hilo lilisababisha kujiuzulu kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Kwa takribani miaka mitano sasa majina ya watu waliochota fedha hizo kupitia Stanbic, yameendelea kuwa siri kubwa, ingawa yapo baadhi ambayo yamekuwa yakitajwa chini chini.

Miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakitajwa ambao vyombo vya dola havijawahi kueleza iwapo viliwakamata kueleza uhusika wao katika sakata hilo lililosababisha mtikisiko mkubwa, ni pamoja na Mbunge mmoja wa CCM ambaye katika utawala wa Serikali ya awamu ya nne alikuwa akihudumu Ikulu.

Wengine wanaotajwa ni mtu anayejitambulisha kama mfanyabiashara anayeelezwa kuwa na ukaribu wa kifamilia na kiongozi mmoja katika Serikali zilizopita.

Wamo pia wanaohusishwa na wamiliki wa moja ya kampuni ambao wanadaiwa kuwa na ukaribu na baadhi ya waliowahi kuwa viongozi wa Serikali katika awamu zilizopita, na wote kwa pamoja wanatajwa kuwa kiunganishi katika kuchukua fedha hizo kutoka Stanbic.

Mtu mwingine anayetajwa kwenye sakata la kuhamisha fedha za Escrow ni Shabani Gurumo ambaye kwa wakati huo alikuwa Mnikulu.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Gurumo, alipohojiwa kwenye Baraza la Maadili, alikiri VIP Engineering and Marketing kumwingizia fedha kwenye akaunti yake na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.

Miongoni mwa watu maarufu walionufaika na mgawo wa Rugemalira ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka (Sh bilioni 1.6) ambaye hivi karibuni ametangaza kuzirudisha ili zimsaidie kutoka Gerezani.

Wengine ni Balozi wa Heshima wa Botswana hapa nchini, Emmanuel ole Naiko (Sh 40, 425,000), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh 40, 425,000), Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja (Sh 40,425,000), Waziri wa zamani na aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Katiba, Paul Kimiti (Sh 40,425,000), Mchungaji Alphonce Twiman (Sh 40,425,000), Askofu Method Kilaini (Sh 80, 850,000) na Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh 40,425,000).

Wamo pia majaji wawili; Aloysius Mujulizi (Sh milioni 40.4) na Profesa Eudes Ruhangisa (Sh milioni 404.2) na wengine.

Aidha wakati Rugemalira akitaka kufumuliwa upande mwingine wa fedha zilizotokana na IPTL na kuanikwa majina waliochota kwa magunia, aliyekuwa mmiliki mwenza wa IPTL, ambaye ameshtakiwa naye, Harbinder Sethi, yeye tayari ameandika barua kwa DPP akikubali kurejesha fedha kulingana na watakavyokubaliana.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Alhamisi wiki hii alimwambia Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shahidi kwamba kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa na anaomba tarehe nyingine.

Naye Wakili wa Rugemalira, Michael Ngalo alidai mteja wake aliandika barua kwenda kwa DPP, lakini hawajapata majibu, hivyo aliomba upande wa Jamhuri kusaidia yapatikane.

Baada ya Wakili Ngalo kueleza hayo, Wakili wa Serikali Wankyo alieleza kwamba ni kweli barua imepokewa na inafanyiwa kazi, majibu atapewa.

Alidai kuhusu upelelezi bado haujakamilika na hawawezi kuahidi ni lini utakamilika.

BARUA YA RUGEMALIRA

Rugemalira aliandika barua Oktoba 4, mwaka huu kwenda kwa DPP na kupokewa Oktoba 5, akiomba aachiwe huru ili aweze kushirikiana na Serikali kupata Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered na washirika wake.

Mshtakiwa huyo ameainisha vielelezo kadhaa vinavyoonyesha Standard Chartered ilivyohusika katika sakata la IPTL.

Miongoni mwa vielelezo hivyo ni gharama zilizokuwa zinatozwa na IPTL dola za Marekani 1.06 kwa kWh ni za chini kuliko zilizokuwa zinatozwa na Songas dola za Marekani 4.31 kwa kWh.

Kielelezo kingine ni barua aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu (BoT) Januari 17 mwaka huu akiomba majina ya watu waliolipwa Sh 144,947,669,844.2 zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow kati ya Julai 5, 2006 na Machi 19 mwaka 2014.

Wakati sakata la Escrow lilivyoingia bungeni mwaka 2014 na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa akauti hiyo kwa maelezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilielezwa kuwa fedha za Rugemalira zilikuwa kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi ambazo baadhi aligawa kwa watu waliotajwa.

 Pia inaelezwa fedha nyingine za PAP, ziliwekwa katika akaunti ya kampuni hiyo ya Sethi ambapo taarifa ya PAC bungeni ilisema zilisombwa kwa sandarusi na watu ambao hawakutajwa na sasa Rugemalira anataka majina ya watu hao kuwekwa wazi.

Pia katika barua yake hiyo kwa DPP, Rugemalira pia anadai alieleza PAP kukiri kulipwa na Benki Kuu Sh 164,513,630,314.15 na dola za Marekani 22,198,544.60 na si Sh 309,461,300,158.27 na dola za Marekani 22,198,544,.60 kama ilivyokuwa katika hati ya mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017.

Aliambatanisha pia nakala ya barua ya BoT yenye kumbukumbu namba NC.130/170/01 iliyoandikwa Februari 18, 2019 ikiwa ni majibu ya barua yake ya Januari 19, 2019.

Kiambatanisho kingine ni cha gazeti la Financial Times la Julai 20/21, 2019 lililotoa taarifa kuwa wadau wameituhumu Benki ya Standard Chartered kwa Serikali ya Marekani kwa kutoa dola bilioni 57 isivyo halali na benki hiyo ilifikia makubaliano na mamlaka za nchi hiyo kwa kukubali kulipa faini ya dola bilioni moja.

“Ninatumaini kwa maelezo hayo yaliyoainishwa katika nyaraka hizi zilizotolewa na ofisi yako kati ya Juni 18, 2019 na Julai 22, 2019 utaweza kutumia mamlaka yako chini ya kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi kuniachia huru katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka 2017 ili niendelee na juhudi zangu za kuisaidia Jamhuri kurejesha zaidi ya Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered,” alieleza.

Alieleza hana tatizo na Jamhuri kwa kuwekwa mahabusu kwa muda wote aliokaa huko, kwa kuwa anaamini hatua hiyo ilichukuliwa kwa Jamhuri kupotoshwa na Benki ya Standard Chartered.

Alimwomba DPP kutumia mamlaka yake aliyopewa katika Kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2016 kuagiza aachiwe huru ili achukue hatua katika kesi zake dhidi ya Benki ya Standard Chartered kupitia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

“Iwapo nitaondolewa mashtaka yanayonikabili, itaniwezesha kuendelea na kesi nilizozifungua dhidi ya Standard Chartered na washirika wake ambapo nadai Sh trilioni 20, kiasi ambacho kitaiwezesha TRA kukusanya kodi  kutoka kwenye hiyo fedha Sh trilioni 6,” alisema.

Katika barua yake, alieleza kuwa viambatishi vingine ni nakala ya tozo iliyokuwa imeandaliwa na Tanesco ikionyesha tozo zilizotakiwa kutozwa na IPTL, ambazo zilikuwa ndogo kuliko za kampuni nyingine.

Ameainisha pia kuwa tozo nyingine ni ya taarifa ya Dk. Camilo Schutte ya Oktoka 12, 2012 kwenda Benki ya Standard Chartered (SCB), Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) Ltd (SCBHK) na Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd (SCBTZ) kuwa iwapo hawataondoa malalamiko yao ya kisheria dhidi ya Tanesco katika kesi ya ICSD namba ARB/10/20, Kampuni ya VIP itaibua madai ya zaidi ya dola milioni 485 kama gharama za usumbufu.

Pia ameambatanisha nakala ya taarifa yake kwa Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd na Jamhuri ya Juni 11, 2013 ikieleza kuwa VIP imechukua hatua ya kukata rufaa kwenye mahakama ya juu ya New York nchini Marekani kwa madai hayo ya dola milioni 485.

Ameambatanisha pia nakala ya Kampuni ya VIP yenye kumbukumbu namba Ref: VIPEM: JB/41/2013 kwenda kwa Gavana wa BoT ya Desemba 5, 2013 kutoiruhusu PAP kulipwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kutoka BoT kwa niaba ya IPTL.

Nyingine ni nakala ya barua yenye kumbukumbu namba NC.53/135/085 ya Desemba 12, 2013 kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndulu ikimweleza Rugemalira kuwa kwa hati ya mahakama iliyotolewa Septemba 5, 2013 Serikali na IPTL malipo yote yameshatolewa kwenye akaunti ya Escrow na kuhamishiwa IPTL Novemba 28, 2013.

MASHTAKA YANAYOWAKABILI

Vigogo hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Juni 19, 2017, wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Rugemarila na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Wanakabiliwa na mashtaka ya  kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi. Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh bilioni 309.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles