25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

WAKULIMA WA KARANGA WATAKA VIWANDA VYA MAFUTA

Na FLORENCE SANAWA-MTWARA


WAKULIMA wa karanga mkoani Mtwara, wameiomba Serikali iwajengee viwanda  vya kukamua mafuta ya kula  ili kuongeza thamani ya zao hilo.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, mkazi wa Kijiji cha Likokona wilayani Nanyumbu, Mkoa wa Mtwara, Zuberi Matuli, alisema kuna haja kwa Serikali kusaidia katika hilo kwa kuwa wamekuwa wakivuna karanga nyingi zisizokuwa na faida.

“Mimi mwenyewe ni mkulima na nimekuwa nikivuna magunia zaidi ya 12 kila mwaka, lakini faida ya zao hilo siioni kwa sababu hakuna soko la uhakika.

“Yaani kitendo cha kutokuwapo kwa soko la uhakika, kimeturudisha nyuma kimaendeleo, jambo ambalo linatufanya tuanze kuiomba Serikali itusaidie kuanzisha viwanda vya aina hiyo.

“Nimeyasema haya kwa sababu naamini Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda na lazima sasa iwekeze kwenye viwanda vya kukamua mafuta ili kuweza kupunguza uingizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.

Naye mkulima mwingine Abillah Nyilenda, mkazi wa Kijiji cha Maugula wilayani Masasi, aliwapongeza watafiti kutoka Taasisi ya Kilimo ya Naliendele iliyofanya utafiti wa kuzalisha mbegu bora za karanga, lakini akasikitishwa na ukosefu wa soko wa zao hilo.

“Binafsi sioni sababu ya kuendelea kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi wakati Naliendele imeonyesha uwezo wa kufanya vizuri katika ufafiti wa mbegu za kukamua mafuta na hivyo kuwa na tija kwa wakulima,” alisema Nyilenda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nanyumbu, Hamisi Damumbaya,  amekiri wilaya hiyo kufanya vizuri  katika uzalishaji wa zao la karanga huku akionyesha wasiwasi unaowarudisha nyuma wakulima kuwa ni ukosefu wa masoko.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Naliendele, Dk. Omar Mponda, alisema mbegu zilizofanyiwa utafiti na taasisi hizo zimeonyesha mafanikio na hivyo wakulima wanahitaji soko kwa ajili ya zao hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles