‘MCHICHA BONDE LA MSIMAZI UNA KEMIKALI ZA SUMU’

0
1079

Na ASHA BANI, Dar es Salaam


NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, amesema kuna hatari ya wananchi kuathiriwa na maji ya Bonde la Mito ya Msimbazi na Kibangu kutokana na kemikali za sumu zinazotoka viwandani kutiririshwa katika mito hiyo.

Kwa sababu hiyo, Mpina ametoa maelekezo kwa uongozi wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuchukua sampuli za maji hayo kufahamu madhara yake.

Naibu Waziri aliyasema hayo jana baada ya kutembelea maeneo ya viwanda vilivyopakana na mabonde hayo kujionea hali halisi.

Alieleza kushutushwa na hali hiyo na kusema kuwa amepata shaka na maji hayo.
Mpina pia aliliiagiza NEMC kupitia mikataba ya Kiwanda cha Anbangs kinachotegeneza mifuko ya salfeti (viroba) na kama hakina kibali kifungwe ndani ya wiki moja.

Katika ziara hiyo, aliwashuhudia wananchi wakiendelea na shughuli za kumwagilia mboga mboga zinazolimwa katika mabonde hayo ambazo huuzwa mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam.

“Kila aina ya sumu ya viwandani inamwagwa katika mabonde hayo na maji hayo ndiyo yanatumika kuendesha shughuli za binadamu ikiwamo kumwagilia bustani za mbogamboga zinazolimwa kwenye mabonde hayo,” alisema.

Akiwa katika Mtaa wa Mivinjeni Sukita, Mpina alisema wanaendelea na juhudi za kuhakikisha hakuna viwanda au watu watakaotiririsha majitaka katika mito hiyo na watakaobainika watachukuliwa hatua za sheria.

Awali, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Barua Mwakilanga alisema wamechimba visima viwili na kununua pampu moja ya kuvutia maji kwa ajili ya wakulima kuepuka kutumia majitaka hayo.

Alisema wanahitaji matenki mawili ya lita 10,000 kila moja yaweze kutumiwa na wakulima hao na Mpina aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here