|Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Wakili Jeremiah Mtobesya, anayewatetea viongozi tisa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, amejitoa katika kesi hiyo baada ya mahakama kukubaliana na upande wa jamhuri kwamba washtakiwa wasomewe maelezo ya awali leo wakati leo kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.
Amedai akiendelea kuwatetea washtakiwa hao, haki haitatendeka.
Upande wa Jamhuri haukuwa na pingamizi kwa uamuzi wa Mtobesya ambapo baada ya kujitoa alibeba kila kilicho chake mezani na kutoka nje ya chumba cha mahakama.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Wengine ni Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na Mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa Kinondoni Mkwajuni walikiuka tamko la kuwataka kutawanyika.