23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Wajumbe watatu wa baraza la ardhi na nyumba wala kiapo mbele ya RC Mhandisi Gabriel

 Na Clara Matimo- Mwanza

Wajumbe watatu wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe na Mkoa wa Mwanza  wameapishwa leo Machi 15 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,  ofisini  kwake huku akiwataka kufanya kazi kwa weledi kuepuka vishawishi vya rushwa, kwani kuna watu ambao watajaribu kuwarubuni ili kupindisha haki.

Mjumbe wa baraza la ardhi na Nyumba  la Wilaya na Mkoa wa Mwanza, Blandina Limihagati , akila kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel,  zoezi hilo limefanyika katika ofisi za mkoa huo, mwenye suti nyeusi ni Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe, Kato Conrad, Picha na Clara Matimo.

Pia ametoa rai kwa halmashauri zote za mkoa huo kuhuisha mabaraza ya ardhi ya kata na vijiji yaliyomaliza muda wake na kutoa elimu kwa wajumbe wa mabaraza hayo ili wajue majukumu yao pamoja na kuendelea  kutenge bajeti kwa ajili ya kuwawezesha washauri kupata vitendea kazi ikiwemo shajara na usafiri.

“Wajumbe mlio kula kiapo leo  fanyeni kazi   kwa weledi kuepuka vishawishi vya rushwa mtaingia kwenye migogoro ambayo wenye fedha wanataka kuwadhulumu wanyonge wasio na fedha mjue hilo lipo katika masuala ya kutafuta haki ninyi msimamie haki, mumtangulize Mungu kwenye kufanya maamuzi yenu na mfuate kanuni, taratibu na sheria ili kujenga imani kwa jamii mkawe  faraja kwao na siyo kukuza migogoro  na kuchelewesha upatikanaji wa haki,”amesema na kuongeza

“Tambueni kwamba kutokana na ongezeko la migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi katika mkoa huu serikali iliona upo umuhimu wa kuanzisha mabaraza ya ardhi  na nyumba ya wilaya katika wilaya za Mwanza, Ukerewe na Sengerema na hivyo kuwa na jumla ya mabaraza matatu katika mkoa wetu lengo ni kuhakikisha migogoro hiyo inatatuliwa,  jamii itakiheshimu chombo chenu endapo  ninyi mtatenda haki,”alisisitiza Mhandisi Gabriel.

Aidha amewataka watumishi   wa mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya waendelee  kutimiza majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo na itakayokuwa inatolewa ili kuboresha utoaji wa huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi na kuhakikisha mashauri yanasikilizwa na kuisha katika kipindi kisichozidi miaka miwili tangu shauri kufunguliwa katika baraza maana wajibu wa mkoa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za ardhi zinatolewa kwa weledi na uadilifu.

“Lakini kama mkisikiliza vizuri kwa kuzingatia weledi mkapata ukweli yawezekana mkatumia muda mfupi zaidi ili kuondoa changamo hiyo maana idadi ya migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi imeendelea kuongezeka siku hadi siku,”amesema mkuu huyo wa mkoa.

Pia amewaasa  wananchi wa Mkoa wa Mwanza  kuendelea kutumia huduma za mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ambayo washauri wake wameapishwa leo ili waweze kupata ufumbuzi wa migogoro yao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wao wajumbe walioapishwa  ambao ni Blandina Limihagati wa baraza la ardhi na nyumba Wilaya na Mkoa wa Mwanza,  Sijo Maira na Muyengi Munubi wa baraza la ardhi na nyumba wilaya ya  Ukerewe wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa kutenda haki ili kutokumuangusha Waziri wa Wizara hiyo, Dk.  Angeline Mabula  kwa kuwateuwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti  na waandishi wa habari baada ya kula kiapo wajumbe hao  wamesema hawatampendelea mtu yeyote katika kutoa maamuzi watatekeleza majukumu yao kwa uaminifu , uadilifu na utiifu  pia kwa kusimamia sheria.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Ukerewe, Kato Conrad, amesema wajumbe hao watawasaidia kusikiliza migogoro ya wananchi  itokanayo na matumizi ya ardhi na kuamua mashauri yao kwa wakati kama kanuni zinavyowaelekeza  hasa ikizingatiwa kwamba  wao ni wenyeji wa maeneo ambayo yanabishaniwa mbele  ya baraza hata kama   masuala ya mila na tamaduni yakiibuka mahakamani.

Mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ni miongozi mwa vyombo vilivyoundwa chini ya kifungu cha 167 cha sheria ya ardhi sura ya 113 kwa ajili ya kusikiliza na kuamua migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi nchini uanzishwaji wa mabaraza hayo  unazingatia sheria ya mahakama za ardhi sura ya 216 kifungu cha 22(1).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles