29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAJASIRIAMALI WASHANGILIA BOMBA LA MAFUTA, VIJANA BADO WAONA GIZA

 

Na WAANDISHI WETU


 

WAJASIRIAMALI katika Jiji la Tanga, wanaamini ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi jijini humo, utawasaidia kuongeza wateja na hivyo kipato chao kuongezeka.

Mradi huo wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilomita 1,443, unatarajia kutengeneza ajira 10,000 wakati wa ujenzi wake na ajira 1,000 baada ya kukamilika.

Wanasema kwa sasa biashara zao zimekuwa hazifanyi vizuri kutokana na hali ngumu inayowakabili wakazi wengi wa Jiji la Tanga.

Abdallah Rajabu, ambaye ni mfanyabiashara ya matunda katika soko la Mgandini, anasema biashara yake imekuwa si nzuri kutokana na hali ngumu ya maisha kwa wananchi wengi.

“Hali kwa sasa ni ngumu. Lakini nina imani kuwa ujenzi wa bomba utakapoanza, mzunguko utakuwa mkubwa,” anasema.

Anasema Mgandini ndiyo soko kubwa kwa Tanga, hivyo wafanyakazi watakaokuwa kwenye mradi huo watalitumia kupata mahitaji yao ya vyakula, jambo litakaloongeza mzunguko wa fedha.

Naye Hamisi Mrisho ambaye ni muuzaji wa mboga mboga, anasema: “Biashara si nzuri sana ingawa tunamshukuru Mungu kuwa riziki tunaipata.

“Ujenzi ukianza tunatarajia kupata wateja zaidi, wageni na wenyeji, pia kipato cha wakazi kitaongezeka kutokana na kupata ajira.”

Simoni Chitage ambaye ni mfanyabiashara wa nyama katika soko hilo anasema: “Watu wengi hawana pesa kwa sasa, tunachopata ni hela ya kula tu.

“Binafsi naamini ujenzi wa bomba ukianza, tutapata wateja zaidi na kuweza kujiongezea kipato ambacho kitatusaidia kufanya mambo mengine ya kimaendeleo kama kujenga nyumba.”

Wafanyabiashara wa samaki katika soko kuu la samaki la Deep Sea, nao wanaelezea matumaini yao chanya juu ya mradi huo, huku wakiiomba Serikali kuwajengea mazingira mazuri ya biashara, ikiwamo soko la kisasa ili wafanye biashara zao vizuri zaidi.

“Samaki ni kitoweo muhimu na kwa kuwa hili ndilo soko kubwa, watakaokuwa wanafanya kazi kwenye ujenzi wa bomba wakitaka kitoweo hiki ni lazima wafike hapa. Cha msingi ni Serikali kutujengea soko zuri ili kuwavutia wateja wa aina zote,” anasema Ustaadhi Kitogo.

Kitogo anasema ukiachana na kufaidika na ongezeko la wateja, vijana wengi wanaokaa vijiweni au maskani kutokana na kutokuwa na kazi, watapata ajira na hivyo kuweza kuendesha maisha yao na kuepukana na utegemezi.

“Ujenzi huu utakuwa na manufaa makubwa sana pia kwa wakazi wa eneo ambalo mradi unapita. Maisha ya wakazi wa eneo la mradi ni duni sana.

“Mradi huu utaweza kusaidia kuwa chachu ya maendeleo kupitia fursa mbalimbali zitakazojitokeza na kikubwa tu ni wakazi wa maeneo yatakayopitiwa na mradi kujituma kufanya kazi,” anasema.

Diwani wa Kata ya Majengo, Selemani Mbaruku, anasema wamekuwa wakiwapatia taarifa wananchi wao ili waweze kujiandaa kutumia fursa zitokanazo na ujenzi wa bomba hilo.

“Mara kwa mara tumekuwa tukiwaambia wananchi wetu kinachoondelea ili waweze kushiriki moja kwa moja katika fursa zitakazojitokeza pindi ujenzi utakapoanza. Tunashukuru kuwa wengi wameonyesha mwitikio mkubwa,” anasema.

 

Wanachofikiria vijana

Juma Mbaruku (23) ni kijana mchangamfu na mwenye uwezo wa kujielezea kwa ufasaha, aliyeanza shughuli za uvuvi tangu akiwa na miaka 16.

“Kazi tunayofanya ni ngumu na hatari pia. Tunalazimika kuifanya kazi hii kwa kuwa hatuna namna nyingine ya kujipatia kipato,” anaeleza.
Anasema  kipato anachopata kutokana na shughuli yake ya uvuvi ni kidogo na hakitoshelezi mahitaji yake ya kawaida kama kijana.

Pamoja na kuwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta upo kijijini kwake, Mbaruku haamini sana kama unaweza kubadilisha hali yake ya maisha.

“Mimi elimu yangu ni darasa la saba na sina fani yoyote ile. Kazi ambayo naweza kufanya katika mradi huu pengine ni kama za saidia fundi tu,” anaeleza.

Kuhusu viongozi kuwaandaa kupata fursa kwenye mradi huo, anadai: “Viongozi wa kijiji zaidi mno walichokifanya ni kuwapunja wakazi wa hapa fidia zao.

 

“Wanakijiji kwa ujumla hawajaufurahia sana mradi huu kutokana na kasoro zilizojitokeza wakati wa ulipaji fidia. Watu walitaka kuonyesha mabango kuelezea kutoridhishwa kwao wakati wa uzinduzi wa ujenzi, lakini walikatazwa.”

Naye Ali Ramadhani, anasema anausubiri ujenzi huo wa bomba la mafuta uanze, akitumaini kuwa huenda ukabadilisha hali yake ya maisha.

“Mimi sina fani, lakini nipo tayari kufanya kazi yoyote ile, ilimradi niweze kujipatia kipato kitakachosaidia kuendesha maisha yangu,” anasema.

Nyumbwe Abdallah, anasema ingekuwa ni vyema kama Serikali ingefanya utaratibu wa kuwaanda vijana kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi mdogo mdogo ili waweze kunufaika na mradi huo mkubwa.

“Vijana wengi hapa kijijini hawana fani. Kama kweli Serikali ina nia ya kutufanya tunufaike na mradi huu, ingetupatia mafunzo madogo madogo,” anaeleza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles