Na KULWA MZEE DAR ES SALAAM
Mbunge Mteule wa Ukonga, Mwita Waitara (CCM) amempongeza Rais John Magufuli kwa kazi aliyoifanya kwa miaka mitatu aliyokuwa madarakani na amemshauri kuwabeza wale wanaompinga kwa sababu watamkwamisha.
Amewataka wapinzani kuiga mfumo wa CCM wa cheo kimoja mtu mmoja na viongozi wa juu kubadilika kila wakati unapofika badala ya viongozi wao kung’ang’ania madarakani miaka nenda rudi kana kwamba wao ndiyo wenye mawazo mazuri kuliko wengine.
Waitara aliyasema hayo jana katika ofisi za chama hicho wilayani Ilala alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema Serikali ya awamu ya tano ni mwendelezo wa Serikali zilizopita, kuna mabadiliko mengi Rais Magufuli ameyafanya ya kuweka sawa mfumo wa uchumi i kuhakikisha fedha za Watanzania zinadhibitiwa na wale wanaofanya ubadhirifu wanachukuliwa hatua.
“Watumishi wanapata mishahara lakini baadhi ya watu wanalalamika hali ngumu, inaonyesha kwamba watu walikuwa wanapata fedha nyingi kwa njia isiyo halali.
“Hii njia isiyo halali ndiyo Serikali imedhibiti fedha za Watanzania ziko katika mikono salama.
“Elimu bure imefanya watoto wengi wamepata nafasi ya kwenda shuleni, hivi sasa kuna haja ya kuwashawishi wanafunzi kusoma sayansi ili kupata walimu wa masomo hayo ambao kwa sasa hawatoshi,”alisema.
Alisema anaunga mkono Serikali kwa kusimamia rasilimali zake, watu wanaokwenda kinyume lazima wawajibishwe ili kufundishana nidhamu na kwamba wanawajibishwa bila upendeleo.
Alimshauri Rais Magufuli kuweka pamba kwenye masiki na asisikie maneno ya wanasiasa walioshindwa watampoteza kwa sababu mwaka 2020 Watanzania wanataka ahadi zilizotolewa ziwe zimetekelezwa.
Alisema anafurahishwa na utaratibu alioukuta katika mgawanyo wa vyeo ndani ya CCM ambako mtu mmoja cheo kimoja hakuna uonevu uliokuwa unatokana na mtu mmoja kuwa na cheo zaidi ya kimoja.
“CCM viongozi wanabadilika, alikuwa Nyerere, akafuatia Mkapa, akaja Kikwete na kisha akaingia Magufuli lakini upinzani miaka nenda rudi viongozi ni wale wale, Profesa Lipumba (CUF) na Katibu Mkuu wake Maalim Seif , ina maana wengine hawana akili?
“Mkibadilisha uongozi mtapata mawazo mapya , kwa mtindo huo mlionao mkisubiri kuitoa CCm madarakani mtasubiri sana,”alisema.
Alimtaka Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema) na wengine kusoma alama za nyakati, wasipofanya hivyo watapata shida katika siasa.
Alimpongeza Rais Magufuli kushiriki katika Kongamano la Uchumi na Siasa na itatokea akaitwa katika mijadala mingine ya wazi aende.
“Usipokuwa na vipaumbele huwezi kupiga hatua, kuna mahitaji mbalimbali ikiwamo kujenga maabara.
“Kuna jambo gani kubwa lilikwama sababu ya Katiba, itumike hii hii, Katiba ni muhimu itaboreshwa kadri siku zinavyokwenda,”alisema.
Alisema Rais anafanya vizuri katika siasa za Tanzania kwa kudhibiti rushwa ambayo kwa sasa imehamia kwa wengine.