Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema jumla ya wahudumu wa afya 137,294 wa ngazi ya jamii wataajiriwa na kuwajengea uwezo katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Hayo ameyasema leo Januari 31,2024 wakati wa uzinduzi wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii uliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema ni lazima kuweka mfumo mzuri wa kuratibu wa shughuli za mpango huo na kuhakikisha taarifa za utekelezaji zinapatikana ikiwemo kutumia mifumo ya kidijitali.
“Katika kutekeleza mpango huu Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi bilioni 899.473 kwa kipindi cha miaka mitano na
kiasi cha bilioni 99 .678 ambazo zitahitajika katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji kwani uwekezaji huu ni mkubwa sana ambao unahitaji rasilimali watu,” amesema Dk.Mpango.
Ameeleza kuwa mpango huo utafanyika katika kipindi cha miaka mitano kwa awamu ambapo katika mwaka wa kwanza (2023/24) zaidi ya wahudumu 28,000 watafikiwa na na wahudumu 27,324 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2024/25 hadi 2027/28.
Amesema mpango huo ambao umezinduliwa leo ambapo wahudumu wa afya ngazi ya jamii watapata aina nne za mafunzo ambazo ni elimu ya afya, huduma za afya kinga huduma tembezi na mkoba na baadhi ya huduma za tiba na kabla ya kutoa vifaa vya kutatua changamoto mbalimbali za afya nchini.
Amesema mambo ambayo yapewe kipaumbele pamoja na lishe, afya ya mama, mtoto, vijana na uzazi wa mpango, magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, usafi wa mazingira, magonjwa ya mlipuko na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema utekelezaji wa mpango huo unazingatia kanuni taratibu na miongozo iliyopo.
Dk. Mpango amewaelekeza viongozi wote wanaohusika katika ngazi zote kuhakikisha zoezi la kuwachagua wahudumu hao linafanyika kwa kufuata vigezo na taratibu zilizowekwa ili waweze kupata wahudumu wenye sifa stahiki.
Pia amezisisitiza Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais _TAMISEMI na Mamlaka zingine zinazohusika kuhakikisha kuna usimamizi madhubuti wa mpango huo ili kufikia malengo yake.
“Ni lazima kuweka mfumo mzuri wa kuratibu shughuli za mradi huu na taarifa za utekelezaji zinapatikana,” amesema.
Aidha amesema wanaweza kujifunza uzoefu kutoka visiwani Zanzibar ambao wameanza kusimamia na kutekeleza mradi huo kwa kutumia mifumo ya kidigitali tangu Desemba 16, 2023.
Dk. Mpango ameitaka Wizara ya Afya kutoa hamasa na elimu ya kutosha kwa jamii kuhusu mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili kurahisisha utekelezaji wake.
Dk. Mpango ametoa rai kuwa masuala ya lishe bora na usafi wa mazingira yasiachwe nyuma katika kutekeleza mradi kama njia mojawapo ya kujenga afya na kudhibiti magonjwa ambayo yanatokana na uchafu.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema mpango huo umelenga kupunguza idadi ya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuimarisha huduma za afya kinga pamoja na kuongeza tija na ufanisi katika kutoa huduma za afya kufikia lengo la afya kwa wote.
Ameongeza kuwa utasaidia pia kukabiliana na upungufu wa vituo vya afya hususani katika maeneo ya vijijini.
“Kupitia mpango huu wahudumu wa afya ngazi ya jamii wameweza kuibua magonjwa mbalimbali yanayoikabili jamii kama vile Kifua Kikuu, Kipindupindu na ugonjwa wa Marburg,” amesema Ummy.
Amesema kupitia mpango huo wataweza kupunguza gharama za matibabu kutokana na kutambulika kwa ugonjwa katika hatua za awali zaidi.
Amesema umuhimu wa wahudumu hao ngazi ya jamii ni daraja kati ya vituo vya kutolea huduma na jamii husika kwa kuwa wamekuwa wakitambua mapema maradhi yanayojitokeza.
Ummy amesema katika kuchagua wahudumu wa afya ngazi ya jamii suala la wakazi wa eneo husika litazingatiwa ili kuendana na mila na desturi za wananchi wa eneo hilo.