29.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wahandisi,Maafisa Manunuzi wakumbushwa kuchapa kazi, kuepuka hoja za ukaguzi

Na Clara Matimo, Mwanza

Wahandisi na Maafisa Manunuzi wa Halmashauri wamekumbushwa kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya taaluma hiyo ili kupata thamani ya fedha na kuepuka hoja za ukaguzi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza, Amina Makilagi akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo.

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani humo, Amina Makilagi Mei 4, 2023 alipokuwa akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wahandisi wa mikoa na halmashauri pamoja na maafisa manunuzi kuhusu usimamizi wa ujenzi na masuala ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi wa miundombinu ya shule za elimu ya awali na msingi kupitia mradi wa BOOST yaliyokutanisha washiriki 192.

“Ili kupata thamani ya fedha na kuepuka hoja za ukaguzi mnapotekeleza miradi ya ujenzi zingatieni sheria zinazowaongoza ikiwemo sheria ya fedha, sheria ya usimamizi wa fedha za umma, sheria za manunuzi, sheria za fedha za serikali za mitaa na sheria ya bajeti.

“Kanuni na miongozo kama mnavyojua mradi wa BOOST ni lipa kwa matokeo sasa ili mradi huo uweze kufanikiwa na kuwa na tija tunawategemea sana nyie kufanya kazi kwa weledi, mkizingatia taratibu na maelekezo yote na kutimiza masharti na vigeo vya uhakiki vitakavyotumiwa na Wakala Huru wa Uhakiki,” amesema Makilagi.

Sehemu ya washiriki.

Makilagi amesema Serikali inatarajia kujenga jumla ya vyumba 12,000 vya madarasa katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi wa BOOST kwa kuanzia mwaka wa pili wa utekelezaji wa mradi huo wastani wa vyumba 3,000 vitajengwa na inawategemea wahandisi na maafisa manunuzi katika kuutekeleza mradi huo pamoja na mingine ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika mikoa mbalimbali nchini.

“Nampongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kuondoa kero za ufundishaji na ujifunzaji shuleni na kuwekeza katika sekta ya elimu ambapo ametoa fedha zaidi ya Sh bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika shule 1,338 za msingi zilizopo katika mikoa na halmashauri zote nchini . hivyo rai yangu kwenu imarisheni ushirikiano ngazi ya halmashauri pia tekelezeni ujenzi wa miundombinu kwa wakati na kwa ubora mkisimamia ujenzi wa miundombinu hiyo kwa weledi na uadilifu.

“Pia epukeni migogoro ambayo huchangia kucheleweshwa utekelezaji wa miradi vilevile msibadili maeneo ambayo yatapangwa kujengwa shule au ukarabati wa miundombinu maana Ofisi ya Rais TAMISEMI ilishafanya tathmini ya ujenzi wa shule na ukarabati wa mindombinu chakavu maeneo yatakayopewa kipaumbele ni yenye msongamano mkubwa wa wanafunzi, vijiji vyenye ukosefu wa shule, maeneo ambayo wanafunzi wanatembea umbali mrefu na shule za msingi zilizobainika kuwa na uchakavu mkubwa,” ameeleza Makilagi.

Amefafanua kwamba endapo wataona kuna uhitaji wa kubadili maeneo halmashauri inapaswa kuwasilisha maombi hayo kwa Katibu Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia kwa Katibu Tawala wa mkoa ili kupata idhini hiyo.

Awali Mratibu wa Mradi wa BOOST OR- TAMISEMI, Joel Mhoja alimwambia Makilagi kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki hao ili wawe na nafasi ya kusimamia vizuri utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu kupitia mradi huo.

“Washiriki wa mafunzo haya yaliyofanyika kwa siku mbili mkoani hapa wamejengewa uwezo juu ya ramani za mpangilio wa majengo na mapitio yake, utambulisho wa DLI na vigezo vya uhakiki, usalama wa mazingira, tafsiri rasmi ya taratibu za manunuzi na utunzaji wa kumbukumbu za manunuzi,” alisema Mhoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles