27 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAGOMBEA KOROGWE WALALAMIKA KUNYIMWA FURSA KURUDISHA FOMU

|Mwandishi Wetu, Tanga



Baadhi ya wagombea wa upinzani walioshiriki kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa marudio ya ubunge katika jimbo la Korogwe Vijijini, wamelalamikia kitendo cha msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini, Kwame Daftari kwa kushindwa kupokea fomu zao.

Wakizungumza na waandishi wa habari wagombea hao wamesema jana Agosti 20 walifika ofisi za halmshauri hiyo kwa ajili ya kurudisha fomu lakini hadi saa 11 jioni walikuwa hawajakutana na mhusika ambaye wanatakiwa kumkabidhi fomu hizo.

Amina Saguti ambaye alikuwa mgombea wa jimbo hilo kupotia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema amesikitishwa na kitendo cha kutopokelewa fomu yake na msimamizi wa uchaguzi, na kwamba yeye alikuwa na nia ya kuwatumikia wananchi wa Korogwe Vijijini.

“Sisi tulifika asubuhi na mapema saa 5:30 kwenye Ofisi ya Halmashauri, na mgombea wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) ametukuta pale lakini cha kushangaza ni kwamba fomu yake imepokelewa kinyemela huku za kwetu tukiishia kuzungushwa na baadaye tunashangaa ametangazwa kuwa ndiye mshindi jambo ambalo hatukubaliani nalo,” amesema Amina.

Kwa upande wa mgombea wa Democratic Party (DP), Josephine George amesema chama chake kimemteua yeye kuingia kwenye kinyanganyiro hicho wakiamini ana uwezo wa kuwaongoza wananchi wa Korogwe Vijijini na kwamba kitendo kilichotokea ni cha kuwanyima haki wananchi hao.

“Kilichotokea hatukukitarajia kwa kuwa tuliwahi kufika kabla ya mgombea wa CCM, tungewaacha wananchi wenyewe wachague kuliko kilichofanyika ni kuwanyima haki yao ya kikatiba,” amesema.

Aidha, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini Amani Gulugwa amesema tayari Katibu Mkuu wa chama hicho Dk. Vincent Mashinji ameshaandika barua kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi kuhusu mambo mawili, kuitisha kamati ya madili ya uchaguzi taifa na kuitisha kikao cha kumjadili msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ili kuwapa fursa ya wagombea kurudisha fomu.

Akijibu masuala hayo, Daftari amesema yeye alikuwepo ofisini muda wote na fomu aliyoipokea ni ya mgombea mmoja tu wa CCM wengine hakuwaona.

“Nilikuwa ofisini kwangu muda wote na sikuwaona hao wengine nimepokea fomu ya mgombea mmoja hadi muda wa kupokea unakwisha na kama yupo anayelalamika namshauri afuate sheria huo ndiyo msimamo wangu, mimi nimetangaza matokeo kwa mujibu wa utaratibu,” amesema Daftari.

 

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles