Derick Milton, Simiyu
Wafugaji wanaoufuga kwa njia za kienyeji wametakiwa kubadilika katika ufugaji wao na kutumia njia ya uhimilishaji (kuweka mbegu kwa njia ya chupa) ili wanufaike na mifugo yao.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Agosti Mosi na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo, Profesa Elisante Ole Gabriel, wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya wakulima (Nanenane) ambayo kitaifa yanayofanyikia Mkoani Simiyu.
Profesa Gabriel amesema wafugaji lazima waache tabia ya kujidai kuwa wanamiliki mifugo mingi na badala yake wafuge kwa tija, kibiashara na wawe na mifugo bora na siyo bora mifugo.
“Wizara imekuwa na utaratibu wa kuwasaidia wafugaji nchini kwa kuwapatia mbegu bora za kupandikizia mifugo na katika maonyesho hay tumeamua kuyatumia kwa ajili ya zoezi hilo kwa wafugaji wote.
“Niwatake wafugaji waje kwenye eneo letu Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuhimilisha mifugo yao kwa bei ndogo ya Sh 5,000, wajitokeze kwa wingi hasa mikoa ya Simiyu, Mara, Shinyanga na Mwanza kwa ajili ya kupewa mbegu hizo,” amesema.
Amesema kuwa kutumia njia hiyo itawawezesha wafugaji kupata maziwa mengi, nyama nyingi, na ndama atakayezaliwa atakuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa wafugaji hawapati tija kupitia mifugo yao.