Na JANETH MUSHI-ARUSHA
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia wafanyabiashara wawili wakazi wa Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha kwa tuhuma za kuwabaka wanafunzi wanne (majina yanahifadhiwa) wa shule tatu tofauti za msingi,wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka 11 hadi 12.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 30, mwaka jana katika Kata ya Daraja Mbili.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Aloyce January (23) na Daniel William (26) ambao wanadaiwa kuwabaka wanafunzi hao wanaosoma Shule ya Msingi Themi, Daraja Mbili na Uhuru na kuwasababishia maumivu makali katika miili yao.
Alisema kuwa uchunguzi wa awali ulibaini kuwa watoto hao waliitwa ndani ya nyumba wanayoishi watuhumiwa na kuwaambia kuwa wanataka kuwatuma, lakini baada ya kuingia waliwatisha na kuwaambia wasipige kelele na endapo wangefanya hivyo wangewachoma visu.
“Baada ya watoto kutishwa iliwalazimu kunyamaza kimya na kufanyiwa kitendo hicho cha kuingiliwa kimwili na kuwasababishia maumivu makali,” alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema baada ya tukio hilo, taarifa zilifika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na raia wema lilifanya uchunguzi na kuwakamata watuhumiwa hao.
Kamanda Mkumbo alisema kuwa wanafunzi hao walichukuliwa kwa mahojiano na watuhumiwa wapo chini ya ulinzi na kwamba upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.