23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Wadau, TCRA wajadili EPOCA

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

SERIKALI imeleta rasimu ya marekebisho ya kanuni nne za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA).

Kanuni hiyo ni kupata suluhisho la kutenganisha kati ya watoa huduma za maudhui mtandaoni kama chombo cha habari na wale wanaotoa maudhui ambayo hayahusiani na vyombo vya habari.

Kutokana na hali hiyo,Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewakutanisha  wadau wa sekta ya mawasiliano na habari jana jijini hapa, kujadili na kutoa maoni kuhusu  kanuni  hizo  nne ambazo ni  kanuni za leseni, kanuni za maudhui mtandaoni, kanuni za miundombinu ya utangazaji kidijitali na kanuni za maudhui ya redio na runinga.

Wadau mbalimbali waliotoa maoni kuhusu rasimu ya kanuni hizo ni pamoja na Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CORI), Baraza la Habari Tanzania (MCT), MISA Tanzania, Umoja wa Makampuni ya Simu Tanzania (TAMNOA), Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Wamiliki wa Ving’amuzi na Jukwaa la Wahariri Tanzania.

Akizungumza wakati wa  mdahalo huo wa kutoa maoni  Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Philip Filikunjombe, amesema kuwa maboresho ambayo wadau wanatolea maoni  yataleta mabadiliko katika sekta ya mawasiliano na habari kwa kutenganisha kati ya watoa huduma za maudhui mtandaoni kama chombo cha habari na wale wanaotoa maudhui ambayo hayahusiani na vyombo vya habari.

Dk. Filikunjombe amesema kuwa maboresho hayo yataondoa sintofahamu ya nani anatakiwa kupatiwa leseni ya kuweka maudhui mtandaoni pamoja na kushusha ada ya leseni hizo.

Amesema  maombi ya leseni kwenye rasimu ya hiyo imeshuka kutoka shilingi laki moja hadi 50,000  na ada ya leseni kwa mwaka imeshuka kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki 5 kwa mwaka.

Aidha amezungumzia kanuni zilizopo kwa sasa zinawataka watoa huduma wa redio na

runinga kuomba leseni ya kutaka maudhui yaleyale kuonekana mtandaoni lakini rasimu hiyo ya maboresho ya kanuni hawatatakiwa kuomba leseni tena ili vipindi vyao kuonekana kupitia mtandao.

Dk. Filikunjombe amezungumzia maboresho ya kanuni hizo kuwa yanaenda kupunguza ada ya leseni ya kurusha matangazo ya redio na runinga kwa asilimia 30 na kuruhusu vituo vya redio na runinga kujiunga na vituo vingine kurusha maudhui yao bila kupata kibali kutoka TCRA isipokuwa watatakiwa kupeleka mpangilio wa vipindi unaoonesha kuwa atajiunga na kituo kingine.

Naye,Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Jim Yonazi amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuwaita wadau hao ili kupata maoni yao kwasababu wao ndio watekelezaji wa kanuni hizo.

Dk. Yonazi  amewaeleza wadau hao kuwa matamanio ya Serikali ni kuboresha mazingira ya watoa huduma za mawasiliano na habari nchini ili wananchi waweze kunufaika na kufaidi bidhaa na huduma bora za mawasiliano.

Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT),Samweli Nyalla amesema ni lazima maoni yao yachukuliwe na yafanyiwe kazi kwani wao wapo katika fani hiyo kwa muda mrefu na wamekuwa na mambo yao ambayo hayafanyiwi kazi ikiwemo mikataba ya uwekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles