27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Wasichana wapewa vyerehani, mafunzo kutimiza ndoto

Na Derick Milton, Simiyu.

Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Restless Development, wametoa vyerehani pamoja na mafunzo ya ushonaji kwa wasichana kutoka Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ambao walipoteza ndoto zao baada ya kupata ujauzito katika umri mdogo.

Wasichana hao wapatao 11, wapo ambao walishindwa kuhitimu masomo yao baada ya kupata mimba wakiwa shuleni, hivyo pamoja na vyerehani wamepewa mafunzo ya kushona nguo kwa  mwezi mmoja.

Akizungumza katika hafla ya  kuhitimu mafunzo hayo, Meneja wa SIDO mkoa huo,  Athanas Moshi amesema kuwa licha ya kushindwa kutimiza malengo yao bado kupitia mafunzo wanaweza kuyafikia.

Amesema SIDO pamoja na Restless Development waliamua kutoa mafunzo kwa wasichana hao, ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuwaeleza kuwa wanaweza kufikia malengo yao kwa njia nyingine tofauti na waliyokuwa nayo.

“Baada ya kuhitimu mafunzo haya, wataendelea kufundishwa kwa muda wa wiki mbili ili waweze kufahamu vizuri zaidi, lakini tumewaeleza kama wataweza kuunda vikundi tutawakopesha ili waweze kujiendeleza zaidi,” amesema Moshi.

Amesema kupitia mafunzo hayo, wasichana hao wanao uwezo mkubwa wa kujiajiri ikiwa wataweza kutumia vizuri maarifa ambayo wamefundishwa pamoja na mtaji wa vifaa ambavyo wamewapatiwa.

Amesema kuwa kila msichana amepatiwa cherehani moja ya kisasa, huku akiwataka kwenda kuunda vikundi kwani SIDO ipo tayari kuwalipia eneo la kufanyia kazi ikiwa pamoja na kuwasaidia kupata mtaji.

Akizungumza kwa niaba  ya wasichana hao, Lusia Limbu amesema kuwa kupewa mafunzo hayo pamoja na vifaa ni ukombozi mkubwa kwao pamoja na familia zao kwani wataweza kujiajiri wenyewe.

Wahitimu hao wamezishukuru taasisi hizo Restless Development pamoja na SIDO kwa mafunzo ambayo yanakwenda kuwaondoa katika umaskini, huku wakiiomba serikali kuwashika mkono kuwapatia mtaji wa kutosha.

Mwakilishi wa Restless Development Mkoa wa Simiyu, Maria Madunga amesema lengo la taasisi hiyo kufadhili mafunzo na utolewaji wa vyerehani hivyo ni katika kuhakikisha wasichana hao wanafikia malengo yao.

Amewataka wasichana hao kutumia vyema mafunzo hayo, kuhakikisha wanajiendeleza, kujituma katika shughuli za ujaslimali ili waweze kufikia malengo ambayo wamekusudia.

Akifunga mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya hiyo, Lupakisyo Kapange, amewataka wasichana hao kutunza vifaa walivyopewa na kufanya kazi iliyokusudiwa huku akiwaasa kuwa wakumbuke bahati haiji mara mbili.

Amesema kuwa licha ya wao kuona ndoto zao zimepotea, lakini kupitia mafunzo hayo wanayo nafasi kubwa ya kubadilisha maisha yao na kuweza kufanya vizuri hadi kuwapita wale ambao waliendelea na masomo.

Aidha ameitaka SIDO kuhakikisha inawafutilia wasichana hao pindi watakapoanza kujitegemea ili kuona kama mafunzo waliyopewa yamebadilisha maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles