30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wadaiwa sugu wa mapato ya Manispaa Tabora kusakwa

Na Allan Vicent, Tabora

Halmashauri ya Manispaa Tabora inatarajia kuendesha msako maalumu kwa wadaiwa sugu wa mapato yatokanayo na ushuru ili kila mmoja alipe madeni yake, na watakaoshindwa kulipa watachukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yamebainishwa leo na Mkuu wa wilaya ya Tabora Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Komanya Kitwala alipokuwa akiongea na MtanzaniaDigital ofisini kwake.

Amesema licha ya wadaiwa hao kutakiwa kulipa madeni yao kwa wakati au kupunguza hadi watakapomaliza baadhi yao wamekuwa wakikwepa na wengine kutotoa ushirikiano jambo linalopelekea halmashauri kukosa mapato.

Amesisitiza kuwa mapato ya halmashauri ndiyo yanayofanikisha utekelezaji miradi ya maendeleo ya wananchi, hivyo hawezi kukubali watu waendelee kulimbikiza madeni tu pasipo kulipa.

Kitwala amebainisha kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa hawatekelezi wajibu wao ipasavyo kwa kutofuatilia na kuchukua hatua stahiki kwa wale wote wanaokwepa kulipa mapato ya serikali, huku akionya kuwa Mtendaji yeyote atakayebainika kuwa chanzo cha upotevu wa mapato hayo atawajibika.

“Tutafanza oparesheni maalumu ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wote katika maeneo mbalimbali ya manispaa, naomba kila mdaiwa sugu ajisalimishe mapema na kulipa deni lake kabla ya kuchukuliwa hatua,” amesema.

Kwa upande wake Meya wa Manispaa hiyo, Ramadhan Kapela amesema kuwa mapato mengi yamekuwa yakipotea kutokana na baadhi ya Watendaji wasio waaminifu na kutowajibika ipasavyo, hivyo akawataka kubadilika mara moja.

Amebainisha kuwa madiwani wana dhamana kubwa ya kusimamia mapato ya halmashauri hivyo akawataka kufuatilia zoezi la ukusanyaji mapato kwa Watendaji wa vijiji na kata ili watekelekeze wajibu ipasavyo.

“Miradi mingi inayotekelezwa na serikali inashindwa kukamilika kwa wakati kutokana na ufinyu wa bajeti, hivyo akawataka kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato ikiwemo kufuatilia madeni yote ili yalipwe,” amesema.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini, Emanuel Mwakasaka amewataka madiwani hao kuwa kitu kimoja na kuhakikisha mapato ya serikali yanayokusanywa yanatumika ipasavyo.

Aidha, ameshauri wale wote watakaobainika kukwepa kulipa kodi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao ili kuwezesha miradi mingi zaidi kutekelezwa ikiwemo kuwezesha vikundi vyote vya vijana, walemavu na akinamama wajasiriamali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles