27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

DC Maswa apiga marufuku kilimo kwenye vyanzo vya maji

Na Samwel Mwanga,Maswa

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyonge amepiga marufuku shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji vinavyolindwa kisheria.

Agizo hilo amelitoa jana Desemba 23, katika kikao cha pamoja na wakulima na viongozi wa serikali wa katika maeneo ambayo mto Sola unapita mjini Maswa.

Amesema hawezi kuvumilia kuona watu wachache wanavunja sheria iliyowekwa ya kuwataka kutofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita sitini toka chanzo cha maji na kwamba eneo hilo kuanzia maeneo ya Mwanguhi, Madeco farm, Binza na Sola baadhi ya watu wasioheshimu sheria za nchi wameamua kufanya shughuli za kibinadamu hasa kilimo jambo ambalo hawezi kulikubali.

Amesema mto huo ni miongoni mwa vyanzo vya maji vinavyopeleka maji kwenye bwawa la New Sola lililoko kwenye kijiji cha Zanzui wilayani humo na ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji huo na vijijini 11.

Kaminyoge amewataka watu wote waliolima mazao yao katika eneo hilo kuacha mara moja kuendeleza shughuli za kilimo kinyume cha hapo ameiagiza mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa)kuwachukulia hatua za kisheria watu wote wakakaokaidi agizo hilo.

“Mimi ndiye msimamizi wa sheria katika wilaya hii na kuhakikisha masuala ya ulinzi na usalama yanakwenda vizuri kuanzia sasa hakuna shughuli za kilimo kufanyika kwenye eneo la vyanzo vya maji, na yale mazao yaliyolimwa kwa sasa ndiyo yanaota hivyo  hakuna kuendeleza hicho kilimo atakayekwenda kinyume Mauwasa washughulikieni kwa mujibu wa sheria.

“Siko tayari kuona watu wachache wanahatarisha maisha ya watu wengi kwani bwawa hili likikosa maji au kujaa tope litazua taharuki kwa wananchi wa mji huu,” amesema.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Raphael Mwita amesema kuwa licha ya kutoa elimu na kuweka mabango yanayokataza kufanyika kwa shughuli za kibinadamu ndani ya chanzo hicho lakini bado wapo watu wachache wakaidi kwa kuvunja sheria.

“Tumetoa elimu ya kutosha juu ya kulinda vyanzo vyetu vya maji ukiwemo huu mto Sola lakini wapo watu wachache wamekuwa wakaidi hata mabango ya kuwazuia wasifanye shughuli za kibinadamu  wameyang’oa na hata vigingi vya kuonyesha mipaka ya mto nayo vimebomolewa, na wengine wanaingiza mifugo kwenye eneo hilo,”amesema.

Ameongeza kueleza kuwa kwa sasa shughuli za kilimo katika eneo hilo zinaendeshwa kwa kasi kubwa na wengine wamejenga nyumba na vyoo vyao vinatiririsha maji machafu ndani ya mto huo unaopeleka maji kwenye bwawa la New Sola.

Diwani wa Kata ya Sola, Masanja Mpiga(CCM) amesema uamuzi uliotolewa na Mkuu wa wilaya ya Maswa ni vizuri wananchi wakaufuata maana eneo hilo linalindwa kisheria hivyo  si vizuri kupingana na sheria za nchi vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles