Na HARRIETH MANDARI- GEITA
WATU wawili wamekufa huku wengine tisa wakinusurika kifo baada ya kuangukiwa na kifusi cha udongo kwenye shimo lenye urefu wa futi 90, wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwenye mgodi wa Bingwa unaotumiwa na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Lwamgasa wilayani Geita.
Waliofariki katika tukio hilo lililotokea juzi Mei 30, mwaka huu usiku ni Leonard Kusekwa (34) na Shida Shija (36), wakazi wa Kijiji cha Nyarugusu wilayani hapa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkaguzi wa Migodi na Baruti kutoka Ofisi ya Ofisa Madini Mkazi, Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel Senge, aliliambia MTANZANIA Jumamosi chanzo cha tukio hilo ni kuyumba kwa mwamba wakati wachimbaji hao wakiendelea kuukarabati ulioporomoka na kuwaangukia, ambapo watu wawili walipoteza maisha.
“Baada ya kupata taarifa hiyo tulifika eneo husika na kubaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kuyumba kwa mwamba,” alisema.
Alisema hali ya kuyumba kwa mwamba hutokea katika mashimo ya uchimbaji hasusani kama eneo linalochimbwa lina maji mengi.
Kwa upande wake, Meneja wa Mgodi na Msimamizi wa Duara hilo lenye Namba 131, Ludelph Zabron, alisema tukio hilo lilitokea baada ya kuyumba kwa magogo ya miti (matimba) yanayotumika kuzuia udongo.
Baadhi ya wachimbaji walionusurika kwenye mkasa huo, wakizungumza na MTANZANIA Jumamosi waliomba kuwepo na kikosi maalumu na vifaa bora vya kuokolea yanapotokea matukio kama hayo.
“Matukio kama haya kwa kweli yamekuwa yakitokea mara kwa mara hasa msimu wa mvua na shughuli kubwa ya kiuchumi katika mkoa huu ni uchimbaji wa dhahabu, hivyo ni muhimu kuwepo kwa kikosi cha aina hiyo,” alisema mmoja wa wachimbaji hao, Richard Paulo.
Naye Wilbert Enock, aliyenusurika katika ajali hiyo alisema ni miujiza ya Mwenyezi Mungu ndiyo iliyowaokoa.
“Kwa kweli nilikuwa nakiona kifo kinanichukua kabisa, kwa sababu lile rundo la udongo lilipoanguka nilijikuta naanza kukata tamaa ya kutoka shimoni nikiwa hai, namshukuru Mungu sana,” alisema.