26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

NISHATI MBADALA NDIYO SULUHISHO LA KUACHA MATUMIZI YA MKAA

JUZI ilikuwa ni uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jiji la Dar es Salaam linaongoza kwa matumizi ya nishati ya mkaa.

Majaliwa anasema kwamba, ripoti ya mazingira ya mwaka 2014, inaonyesha kuwa Dar es Salaam inatumia tani 500,000 ya mkaa kwa mwaka jambo linalohitaji nishati mbadala, vinginevyo kutatokea madhara makubwa hapa nchini.

Pia anasema kwamba, ripoti hiyo inaonyesha hekta 372,000 za misitu hukatwa nchini kwa mwaka, hivyo elimu ya uhamasishaji na teknolojia mbadala ndivyo vitakavyoiokoa misitu hiyo.

Mathalani anasema Msitu wa Kazimzumbwi uliopo Kisarawe, Pwani umeathiriwa kwa sababu ya ukataji ovyo wa miti na asilimia 70 ya mkaa unatumika Dar es Salaam tofauti na vijijini ambako wengi wanatumia kuni zilizokauka na kuanguka zenyewe.

Pamoja na mambo mengine, sisi wa MTANZANIA Jumamosi tunasema kwamba nishati mbadala ndiyo suluhisho pekee la kupunguza ama kuacha kabisa matumizi ya mkaa. Pia tunakubaliana na Majaliwa kwamba ili kuokoa mikoa iliyoathiriwa na ukataji ovyo wa miti, ni vyema mamlaka zinazohusika na utoaji wa vibali vya ujenzi kuhakikisha kuanzia sasa utoaji wa vibali hivyo hasa katika majengo makubwa ya binafsi na Serikali vizingatie mifumo ya usambazaji gesi ili kutokomeza matumizi ya mkaa na kuni.

Kwa sababu tafiti zinaonyesha majengo makubwa mengi yana matumizi makubwa ya mkaa na kuni, hivyo kitendo cha kufunga mifumo ya nishati mbadala kitasaidia kupunguza matumizi hayo.

Pia tunaunga mkono agizo lake la kuwataka wakuu wa mikoa kuanzia sasa wahakikishe wanatembelea taasisi za umma na binafsi ili kuwapa muda maalumu wa kubadili mifumo ya matumizi ya kuni na mkaa kwa sababu itasaidia kuongeza tija ya nishati mbadala na kulinda misitu iliyopo.

Si hivyo tu, pia tunaunga mkono agizo la kutaka teknolojia mbadala zisambazwe nchi nzima ili watumiaji wake wabadilike na mamlaka husika zifanye ukaguzi kila baada ya miezi sita.

Mbali na hayo, pia tumeshtushwa na kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, kwamba kwa siku Dar es Salaam inatumia magunia 300,000 ya mkaa.

Kwamba mbali ya uwapo wa gesi asilia hapa nchini lakini asilimia 90 ya Watanzania bado wanatumia mkaa na Dar es Salaam pekee inatumia asilimia 70.

Kutokana na hali hiyo, tunamshauri January na wizara yake kwamba ni wajibu wao kuendelea kuwaelimisha Watanzania kuhusu namna bora ya kuyatunza mazingira yetu na isisubiri tu hadi wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira.

Kwamba kina January waendelee kupiga kelele na kukemea utumiaji wa mkaa kwa sababu asilimia 70 hadi 80 ya miti inayokatwa inachoma nishati hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles