24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

DAKTARI: DALILI ZA UGONJWA WA LUPUS ZINAFANANA NA UKIMWI

 

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WATU wanaokabiliwa na ugonjwa wa Lupus wanaelezwa kuwa na dalili zote zinazofanana na zile za ugonjwa wa Ukimwi.

Si tu Ukimwi bali pia magonjwa ya akili, figo, mifupa na ubongo.

Hayo yalielezwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo na Lupus (Rheumatorogist), Francis Furia, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ugonjwa huo Dar es Salaam jana.

Alisema ugonjwa wa Lupus mara nyingi husababisha kinga ya mwili ya mgonjwa husika nayo kushuka.

“Ili mtu aelewe jinsi ugonjwa huu ulivyo, ni kama vile jeshi la nchi lenyewe linapaswa kulinda nchi lakini inapotokea jeshi linashambulia nchi tayari ni tatizo.

“Hivyo badala ya ile kinga ya mwili kuulinda inatokea ghafla inaanza kushambulia viungo vyake badala ya kushambulia bakteria au virusi vinavyoingia mwilini mwake,” alisema.

Akifafanua, Dk. Furia ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas),  alisema ugonjwa huo huweza pia kurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kupitia vinasaba.

Alisema tafiti mbalimbali zilizofanyika ulimwenguni hasa Marekani zinaonesha watu weusi (Waafrika) na wenye asili ya Bara la Asia ndio ambao huathirika zaidi na ugonjwa wa Lupus kuliko wazungu.

“Wapo ambao hupimwa hadi mara saba wakidhaniwa ni waathirika lakini kila wakipimwa wataalamu hawaoni kitu na baadaye hugundulika ni ugonjwa wa Lupus,” alisema.

Alisema sasa wanagundulika mapema kwani mifumo ya afya ya uchunguzi imeimarishwa kuliko ilivyokuwa zamani.

“Wiki hii nimeona wagonjwa watatu wakiwamo wakubwa kwa watoto, huonesha dalili mbalimbali na wengine huonesha kama wana magonjwa ya figo au akili, lakini tukiwaona tuna uwezo wa kutambua wanasumbuliwa na Lupus na kwa kutumia vipimo vya kina vya uchunguzi,” alisema.

Alisema wakati mwingine huonesha dalili za saratani ya damu kumbe ni Lupus.

Dk. Rupia alisema tafiti zilizowahi kufanyika nchini Marekani zinaonesha ugonjwa huo hushambulia zaidi wanawake hasa walio katika umri wa kuzaa kuliko wanaume.

“Tafiti zinaonesha kati ya watu wanane hadi 15 wenye ugonjwa huo, mwanamume huwa ni mmoja pekee na waliobaki huwa ni wanawake, aidha, kwa kundi la watoto wenye ugonjwa huo uwiano huwa ni mwanamume mmoja kati ya watu watatu,” alisema.

Alisema inadhaniwa homoni ya kike ya Estrogen huenda ndiyo inayochochea wanawake kupata ugonjwa huo kuliko wanaume.

Alisema tafiti za huko Marekani inakadiriwa kati ya watu 100,000, watu 20 hadi 150 huwa wanaugua ugonjwa huo.

“Hapa Tanzania hatujawahi kufanya utafiti lakini kwa mfano tukitumia takwimu hiyo ya utafiti wa Marekani maana yake ni kwamba kati ya Watanzania milioni zaidi ya 50 itamaanisha kwa makadirio kiasi cha wilaya moja nzima ni wagonjwa wa Lupus, lakini hatuna takwimu halisi kwani hatujafanya utafiti wa kina,” alitoa mfano.

Alisema wagonjwa wengi hugundulika nchini kupitia kwa madaktari wa ngozi na figo.

Alisema watoto huweza kuathiriwa na ugonjwa huo angali wakiwa tumboni mwa mama zao.

Alisema mtu mwenye ugonjwa wa Lupus huwa hawezi kukaa au kutembea juani kwani humchoma ngozi yake na hivyo kupata maumivu.

Akielezea historia ya ugonjwa huo, alisema uligunduliwa na mchungaji mmoja huko Marekani katika karne ya 13 na kwamba hutokana na hitilafu kwenye mfumo wa kinga ya mwili.

Alisema mchungaji huyo aliupatia jina hilo la Lupus kutokana na wagonjwa wengi aliowaona walipata mabaka usoni hali iliyowafanya waonekane kama mbweha.

Alisema baadaye wataalamu waliongeza neno systematic kwani ulionekana kuathiri sehemu nyingine za mwili na si usoni pekee.

“Baadaye tena wataalamu wa afya waliongeza neno jingine Erythematous kwamba huathiri mfumo mzima wa kinga ya mwili na tangu hapo ukatambulika kama Lupus Systematic Erythematous Disease au kwa kifupi Lupus,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles