25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge waicharukia TANESCO

tanesco-logoNa Jonas Mushi, Dar es Salaam

KAMATI ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), imelibana Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO)  kuhusu mikataba mibovu iliyoingia na kampuni za uzalishaji umeme.

Viongozi wa shirika hilo jana waliitwa mbele ya kamati hiyo wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Justine Talikwa na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Mhandisi Felichesmi Mramba ambaye alifuatana na watumishi wengine wa Tanesco.

Wajumbe wa kamati hiyo walidai kwamba shirika hilo limekuwa na madeni makubwa kutokana na kununua umeme kwa gharama kubwa kutoka kwa wazalishaji huku ikiuza kwa gharama ndogo.

Wengine walihoji sababu za shirika hilo kuendelelea na mkataba na Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya IPTL ambayo imeisababishia Serikali hasara kubwa zinazotokana na kulipa gharama za uwekezaji (Capacity Charge).

Mbunge wa Bukene ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo, Suleiman Zeddy (CCM) alihoji kwa nini IPTL inalipwa gharama za uwekezaji, wakati haikuwa na mtaji wa uwekezaji.

Naye Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) alihoji kwa nini TANESCO haikufuta mkataba baada ya IPTL kufunga mitambo dhaifu ya MCD badala ya mitambo ya CCD kwa mujibu wa mkataba.

“IPTL ilikuwa ni kwa lengo la kuzalisha umeme wa dharura na ilitakiwa kufunga mitambo ya CCD lakini wao wakafunga mitambo ya MCD ambayo ni dhaifu,” alisema Kakunda na kuongeza: “TANESCO ingekuwa makini ingetakiwa kuvunja mkataba huo mapema,” alisema.

Aliongeza kuwa Tanesco inatakiwa kujiuliza kama inaona ni sawa kuendelea kuilipa IPTL gharama za uwekezaji.

Aidha Kakunda alihoji kwa nini shirika hilo halikuendeleza mradi wa Stiglas Gorge uliokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 2000 kwa gharama ndogo kuliko ilivyo sasa ambapo Megawati 400 zinagharimu Sh trilioni 15.

Mbunge wa Viti maalumu, Riziki Said Lulinda (CUF), alitaka TANESCO kuleta mikataba iliyoingia na kampuni za uzalishaji wa umeme mbele kamati hiyo ili waweze kuona udhaifu uliopo na kuwachukulia hatua walioingia mikataba hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PIC, Richard Ndasa ambaye pia ni Mbunge wa Sumve alihoji deni la Sh bilioni 682.1 huku yenyewe ikidai Sh bilioni 253.7 kiasi ambacho alisema hata wakilipwa bado hawawezi kulipa deni lao.
Majibu ya TANESCO

Akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe wa kamati hiyo, Talikwa alikiri kuwepo kwa mikataba mibovu ambayo inawasumbua.

Naye Mramba alijibu maswali ya wajumbe hao na kusema shirika hilo limeweza kupunguza hasara kutoka Sh bilioni 179 mwaka 2014 katika kipindi cha miezi 12 na kufikia hasara ya Sh bilioni 35 mwaka jana.

“Suala la kuuza umeme kwa gharama za chini kuliko tunayonunulia halipo chini yetu bali ni EWURA na tukisema tuuze umeme kwa lengo la kurudisha fedha za uzalishaji utakuwa ni ghali sana na ikizingatiwa inagusa wananchi moja kwa moja inaweza kuleta athari kubwa sana,” alisema Mramba.

Kuhusu mikataba ya IPTL alisema si jepesi na lisingeweza kujibiwa wakati huo na kudai kuwa wanatarajia kufanya mazungumzo na kampuni hiyo ili iweze kuharakisha kubadili mfumo wa kutumia mafuta mazito ili itumie gesi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles