24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge tishio wabanwa bungeni

MTZ IJUMAA newfinal.indd* Zitto, Serukamba, Bashe, Zungu, Kubenea, Chegeni, Nyalandu wapelekwa Huduma za Jamii

* Sophia Simba, Kingu, Heche watupwa Kamati ya Ukimwi, Ukawa wapinga

Khamis Mkotya na Elias Msuya, Dodoma

HATIMAYE Spika wa Bunge, Job Ndugai, ametangaza uteuzi wa Kamati za Kudumu za Bunge ambazo zilikuwa zikisubiriwa kwa hamu, huku wabunge machachari wakibanwa.

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamekosoa mpangilio wa wajumbe katika kamati, huku baadhi ya wabunge wenye majina wakijikuta wakitupwa katika kamati tofauti na kile kilichodaiwa kuwa tofauti na matarajio yao.

Katika kile kilichoonekana kuwapo na joto katika uteuzi huo, orodha hiyo ilichelewa kutolewa  kwa vile  wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikwenda White House  kufanya kikao chao (Party Caucus).

Hata hivyo wabunge hao walipofika bungeni   mchana  hawakuweza kupata orodha na kulazimika kurudi katika kikao chao ambako walielezwa kuwa orodha hiyo ingekuwa tayari saa 10.00 jioni.

Lakini  wakati orodha hiyo ikitolewa jana saa 10.30  jioni, wabunge waliokuwapo katika viunga vya Bunge ni wale wa upinzani tu, kwa vile  wabunge wa CCM walikuwa wanaendelea  na kikao chao.

Katika orodha hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), safari hii amejikuta akipangwa katika Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii..

Wengine waliopangwa katika kamati hiyo ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, ambaye awali alikuwa akitajwa kwamba alikuwa akifanya akisaka kwa udi na uvumba, uenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Malisili na Utalii.

Mwingine   katika kamati hiyo ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM) ambaye katika Bunge lililopita alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu.

Wabunge wengine  katika kamati hiyo ni   Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) na Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu (CCM, ambaye Bunge lililopita alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), ambaye katika Bunge lililopita alikuwa Kamati ya Nishati na Madini, safari hii amejikuta akipangwa katika  Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji.

 

Silinde

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa upinzani wamekosoa uteuzi wa wabunge wa upinzani katika kamati za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Wakati kwa mujibu wa kanuni za Bunge, kamati hizo   zinatakiwa kuongozwa na upinzani, lakini wabunge hao wamesema wanaona mchezo mchafu umefanyika  kutokana na  wajumbe wengi wa kamati hizo kutoka upinzani    kuwa wapya.

Akizungumza na Mtanzania, Mbunge wa Momba, David Silinde (Chadema), alisema Kamati za Bunge ni vyombo muhimu katika kujadili mipango ya Serikali, hivyo uteuzi wa wajumbe ni muhimu kuzingatia sifa madhubuti.

“Kwa orodha hii naona kuna mchezo katika kamati zetu zinazotakiwa kuongozwa na upinzani. Kamati hizi za PAC na LAAC wajumbe wengine wa upinzani ni wapya.

“Mimi sijui Spika amezingatia vigezo gani kupanga hizi kamati, kila mbunge hapa ukizungumza analalamika wamewekwa kamati ambazo hawawezi kusaidia kamati vizuri.

“Kwa mtazamo wangu sifa tatu zilipaswa kuzigatiwa; taaluma ya mbunge, uwezo na uozefu. Sasa kwenye kamati kama ya PAC au LAAC unamweka mbunge mpya hapa kuna tatizo.

“Kamati ndiyo kila kitu, kwa sababu hoja zinaanza kujadiliwa huko kabla ya kuingizwa bungeni. Mbunge makini mara kumi akose kikao cha Bunge lakini ahudhurie vikao vya kamati, kwa sababu kamati ndiyo kila kitu, ” alisema.

Mbunge mwingine kutoka Chama cha Wananchi (CUF), ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema; “wamepanga watu ambao ni light (wepesi) mwenyekiti awe ‘kiazi’ halafu makamu mwenyekiti ambaye atatoka CCM anakuwa mtu makini, hapa kuna shida”.

 

PAC

Kwa mujibu wa orodha hiyo, Kamati ya PAC ina wajumbe 23, ambako kati ya hao wabunge kutoka upinzani wapo sita.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Viti Maalumu, Naghejwa Kaboyoka (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Rais Abdallah Mussa (CUF) na Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk (CUF).

Wengine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Yosefa Komba (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Tunza Issa Malapo (Chadema) na Mbunge wa Mwanakwerekwe, Ali Salim Khamis (CUF).

 

LAAC

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ina wajumbe 22, na kati ya hao wabunge kutoka upinzani ni sita.

Miongoni mwao ni Mbunge wa Mgogoni, Dk. Suleiman Ally Yusuf (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema) na Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza (Chadema).

Wengine ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Vedasto Ngombale (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Kiwelu (Chadema) na Mbunge wa Ukerewe, Joseph Mkundi (Chadema).

 

Kamati ya Uwekezaji

Baadhi ya wabunge ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini, walisema kambi ya upinzani imepunguzwa nguvu katika kuongoza kamati baada ya iliyokuwa Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) kurudishwa kwa jina jingine.

Hali hiyo imejitokeza baada ya kuundwa kwa Kamati mpya ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, ambayo inadaiwa kuwa majukumu yake ndiyo yale yaliyokuwa yakifanywa na Kamati ya POAC.

“Katika Bunge la tisa wapinzani tulikuwa tunaongoza kamati tatu, PAC, LAAC na POAC, Bunge la 10 la Spika Makinda, POAC iliunganishwa na PAC wapinzani tukabaki na kamati mbili.

“Safari hii kilichofanyika wamerudisha POAC kwa jina jingine wakaita Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na sasa itaongozwa na CCM, lakini majukumu yake ni yale yale yaliyokuwa yakifanywa na POAC ya kusimamia mashirika ya umma,” alisema mbunge mmoja wa upinzani.

Kamati hiyo ina wajumbe 22, ambao kati ya hao  wabunge kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni 15 wakati wabunge wa upinzani ni saba.

Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo ni Mbunge wa Kondoa Mjini, Edwin Sanda (CCM), Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema).

Wengine ni Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema) maarufu kama Profesa Jay, Mbunge wa Bukene, Selemani Zedi (CCM) na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani (CCM).

 

Kamati ya Ukimwi

Walioteuliwa katika Kamati ya Ukimwi ni Waziri wa zamani wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), Mbunge wa Ukonga, Waitara Mwita (Chadema), Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM).

Wengine ni Mbunge Bumbwini, Mohamed Amour Mohamed, (CCM), Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamadi (CUF), Mbunge wa viti maalumu, Severiana Mwijage (CUF), Mbunge wa Mtambwe Khalifa Mohamed Issa (CUF).

 

Ukawa wakutana

Baada ya kamati za Bunge kutajwa viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) walionekana kutokukubaliana na kuna dalili za kugomea kamati hizo kutokana na kutoridhishwa na jinsi zilivyopangwa.

Ilipofika saa 10 alasiri baada ya kamati hizo kutangazwa, waandishi wa habari waliitwa kwenye ofisi ya kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, lakini baadaye Naibu Katibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika aliwaambia kuwa mkutano huo uliahirishwa hadi leo.

“Tumeona tuahirishe mkutano   na waandishi wa habari kwa sababu hili suala ni kubwa sana. Tutakuwa na kikao cha viongozi wa vyama vya upinzani na baadaye ‘party caucus’ leo au kesho, kwa hiyo tutawaita kesho,” alisema Mnyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles