Na Arodia Peter, Dodoma
KWA mara ya kwanza tangu kuanza kwa Bunge la bajeti wabunge jana walikuwa na msimamo wa pamoja kwa kuyakataa mapendekezo karibu yote ya Serikali yaliyomo kwenye Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2016.
Muswada huo uliosomwa kwa mara ya pili juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, pamoja na mambo mengine ulipendekeza kuondolewa kwa Kamati ya Fedha na Uchumi inayoundwa na madiwani katika halmashauri nchini.
Muswada huo ulipendekeza kamati hiyo ya madiwani isihusike kupokea na kujadili taarifa za matumizi pamoja na michakato mbalimbali ya tenda na badala yake kazi hiyo ifanywe na wakurugenzi pamoja na watendaji wa Serikali pekee.
Katika mjadala huo jana, Waziri Mpango, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju pamoja na Naibu Waziri wa Fedha, Dk. Ashatu Kijaji walipata wakati mgumu kujibu hoja za wabunge ambao walikuwa na msimamo mkali kwa baadhi ya vifungu vilivyopendekezwa na Serikali katika muswada huo.
Hoja nyingine ambayo ilimsumbua zaidi Masaju ni kuhusu marekebisho ya sheria inayotaja wazawa kupata zabuni za Serikali kwa kushirikiana na wageni.
Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka alipendekeza wakandarasi wazawa watambuliwe na sheria ili wasije wakamezwa na wakandarasi wenye mitaji mikubwa.
“ Mheshimiwa mwenyekiti sheria ya zamani ya manunuzi ambayo mmeleta marekebisho haya ilikwishaleta ukakasi mkubwa, vijana wetu wanafanya biashara na serikali, hizi ndiyo ajira zenyewe mwenyekiti, tusipowawekea misingi ya kisheria vijana wetu watakuja kutupwa nje na watu wenye mitaji mikubwa” alisema Profesa Tibaijuka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, pamoja na mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge (CCM) walimpa wakati mgumu, Masaju kwa kupangua vifungu mbalimbali vya marekebisho ya Serikali huku wakiungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge.
Katika mojawapo ya vipengele hivyo vya muswada ambavyo Ghasia alivivalia njuga ni pamoja kile kinachohusu zabuni za ununuzi wa dawa za binadamu lisiingizwe kwenye utaratibu wa kawaida wa tenda.
Badala yake Ghasia alipendekeza sheria iwekwe wazi kwamba dawa zinaweza kununuliwa wakati wowote bila kufuata mfumo wa kawaida wa zabuni ili kuondoa matatizo na ucheleweshaji kwenye michakato wa zabuni.