
Na Asifiwe George, Dar es Salaam
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lisu (Chadema), jana alilala katika Kituo cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutokana na kukataliwa dhamana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mwanasheria wa Tundu Lisu, John Malya, alisema mteja wake amelala Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati, kwa kile kilichodaiwa kutoa maneno ya uchochezi yenye lugha ya kuudhi.
Alisema mteja wake alihojiwa saa tatu na neno kubwa walilomuhoji ni kutokana na kutoa neno la ‘Rais dikteta Uchwara’ na ametoa ufafanuzi kuhusiana na neno hilo na amerekodiwa na polisi.
“Kesho tutarudi tena hapa Polisi kwa ajili ya kupewa maelekezo kwamba anapelekwa mahakamani au ni kitu gani kinaendelea, mawakili wake tupo na tutahakikisha kwamba anapata haki zake za kisheria kwa wakati,” alisema Malya.
Malya alisema kwamba Lissu hakutuma ujumbe wowote wa uchochezi katika mitandao ya kijamii kama inavyodaiwa, kwasababu ukituma ujumbe katika mitandao ya kijamii kwamba mikutano ya kisiasa imezuiliwa hilo si neno baya wala halina uchochezi wowote.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), alisema wamepewa maagizo kwamba Tundu Lissu hawezi kutoka ambapo alimtaka akamtafutie chakula ili aweze kula na kulala.
“Mwelekeo wa nchi si mzuri, polisi, Rais wasifikiri kwamba anawatisha watu kwa bunduki au kulala ndani,ni lazima kama kuna kosa akosolewe,” alisema Lema.