CENTRAL, HONG KONG
MAELFU ya watu jana waliandamana tena Hong Kong wakitaka uhuru wa jimbo hilo ambalo ni sehemu ya China. Maandamano hayo ambayo yanaingia kwenye rekodi ya muda mrefu yameliacha eneo hilo katika makovu makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa watu wake.
Waandamanaji walioandamana jana ambao wengi wao wameonekana wakiwa wamevalia nguo nyeusi wamefanya maandamano katika wilaya ya Tuen Mun na wamesikika wakisema;
“Mapinduzi ya wakati wetu” na “Rejesha Hong Kong”.
Hong Kong imeingia katika mwezi wa nne wa maandamano, ambayo yalianza kwa wananchi kupinga muswada wa sheria unaoelekeza wahalifu wa Hong Kong wapelekwe kushtakiwa China.
Madai ya waandamanaji wa mji huo yamepanuka na sasa wanataka demokrasia zaidi.
Hata hivyo maandandamano ya jana yamehusisha watu wachache ikilinganishwa na mwishoni wa wiki zilizopita.
Katika maandamano hayo hakujaripotiwa vurugu tofauti na siku zilizopita ambapo polisi walilazimika kukabiliana na raia.