Waandamanaji nchini Sudan wametoa wito wa kufanyika maandamano makubwa, wakisisitiza kuwa jeshi halina nia thabiti ya kukabidhi madaraka kwa raia karibu wiki tatu baada ya kuuondoa madarakani uongozi wa Omar al-Bashir.
Wito huo unakuja wakati hali ya wasi wasi ikiongezeka kuhusiana na muundo wa baraza jipya la pamoja kati ya raia na jeshi litakaloiongoza nchi ya Sudan, wakati waandamanaji wakiimarisha vizuwizi nje ya makao makuu ya jeshi katika mji mkuu Khartoum.
Pande hizo mbili zina mambo mengi yanayokinzana kuhusiana na wawakilishi katika baraza hilo jipya ambalo linatarjiwa kuchukua nafasi ya baraza la kijeshi ambalo lilichukua madaraka baada ya kuondolewa madarakani Omar al-Bashir Aprili 11 baada ya maandamano makubwa ya umma kupinga utawala wake wa miongo mitatu.